CRDB YAIKOMBOA SHULE YA PATRICK QORRO, YAKABIDHI VITI NA MEZA 50
...DC KARATU AITAKA BENKI HIYO KUPANUA HUDUMA ZA KIFEDHA KWA WANANCHI, WAKULIMA NA VIJANA
Na Joseph Ngilisho| KARATU
BENKI ya CRDB imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini baada ya kukabidhi viti na meza 50 kwa Shule ya Sekondari Patrick Qorro wilayani Karatu, mkoani Arusha, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufanisi wa wanafunzi darasani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi samani hizo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, alisema benki hiyo imedhamiria kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na jamii katika kuboresha huduma za kijamii, hususan elimu, kwa kutambua nafasi yake katika kujenga msingi wa maendeleo ya taifa.
Sadat alisema kampeni ya Keti Jifunze ni sehemu ya juhudi za CRDB kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia, huku benki hiyo ikiendelea kutoa mchango wake katika shughuli za maendeleo zinazogusa maisha ya wananchi.
Alisema CRDB inaamini kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa, hivyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii inanufaika na huduma na programu zake za uwajibikaji kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dkt. Lameck Karanga, aliipongeza CRDB kwa msaada huo, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuweka mazingira yanayowawezesha wanafunzi kusoma kwa ufanisi.
Dkt. Karanga alisema msaada huo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo na Wilaya ya Karatu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
Hata hivyo, aliitumia fursa hiyo kuitaka CRDB kupanua zaidi wigo wa huduma zake wilayani Karatu kwa kutoa elimu ya fedha na kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na vijana.
Alisema makundi hayo yanahitaji huduma za kifedha zitakazowawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya wilaya.
Msaada huo ni sehemu ya dhamira ya CRDB ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji katika sekta muhimu zikiwemo elimu na afya, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi.











Post a Comment