Ad
Breaking🔥

NDEJEMBI KUFUNGUA JUKWAA LA KIMATAIFA ARUSHA KESHO, WAGENI ZAIDI YA 3,000, NCHI 45 KUKUTANA

NDEJEMBI KUFUNGUA JUKWAA LA KIMATAIFA ARUSHA KESHO,WAGENI  ZAIDI YA 3,000, NCHI 45 KUKUTANA 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

JUKWAA la kimataifa la biashara, teknolojia na usafirishaji wa mazao ya kilimo, HortiLogistica Africa- 2026, linatarajiwa kuifanya Arusha kuwa kitovu cha biashara ya mazao ya kilimo barani Afrika, likitarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Deogratias Ndejembi likiwakutanisha wageni zaidi ya 3,000 kutoka mataifa 45, wakiwamo wanunuzi zaidi ya 150 kutoka masoko mbalimbali duniani.

Jukwaa hilo litakalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha kuanzia Novemba 8 hadi 10 mwaka huu, linatajwa kuwa fursa ya kimkakati kwa Tanzania kufungua masoko mapya, kuvutia uwekezaji na kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mapato ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, alisema jukwaa hilo si maonyesho ya kawaida, bali ni fursa ya kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na usafirishaji wa mazao ya kilimo katika bara la Afrika.

Alisema mkutano huo utawaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wawekezaji, wasafirishaji na watoa huduma mbalimbali, hivyo kuwapa wakulima na wafanyabiashara nafasi ya kupata masoko ya uhakika na kujenga mahusiano ya kibiashara na mataifa mengine.

“Jukwaa hili si maonyesho pekee, bali ni fursa ya kuwaunganisha wazalishaji wa mazao ya kilimo na wanunuzi wa kimataifa, kuvutia mitaji mipya na kufungua masoko mapya kwa wakulima na wafanyabiashara wetu,” alisema Makalla.

Alisema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha matunda, mboga mboga, viungo na maua, hivyo ujio wa wanunuzi na wawekezaji hao ni nafasi ya kuonyesha uwezo huo na kuwavutia kuwekeza katika uzalishaji, uchakataji, uhifadhi na usafirishaji wa mazao.

Makalla alisema jukwaa hilo linaongeza hadhi ya Arusha katika ramani ya kimataifa, baada ya mkoa huo kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa ikiwamo IPU na Commonwealth.

Alisema manufaa ya mkutano huo hayatabaki katika sekta ya kilimo pekee, bali yatachochea shughuli za hoteli, usafirishaji, utalii, biashara na usafiri wa anga kutokana na ujio wa maelfu ya wageni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA), Jacqueline Mkindi, alisema Tanzania inalenga kutumia jukwaa hilo kupanua masoko ya mazao ya bustani katika nchi mbalimbali za Afrika, badala ya kutegemea zaidi masoko ya Ulaya na Asia.

Alisema kwa muda mrefu wafanyabiashara wengi wa Afrika wamekuwa wakielekeza nguvu katika masoko ya nje ya bara hilo, yakiwamo Uholanzi na Dubai, huku wakiacha fursa kubwa zilizopo ndani ya Afrika.

“Tunapoongelea masoko hatuongelei tu Dubai au Uholanzi, tunaongelea pia masoko ya Afrika. Hilo ndilo tunalolilenga na manufaa makubwa yako hapa,” alisema Mkindi.

Alisema jukwaa hilo litashirikisha mataifa 45, yakiwamo zaidi ya 18 kutoka Afrika, likiwaunganisha wazalishaji wakubwa wa mazao ya bustani kama Tanzania, Kenya na Ethiopia na nchi nyingine zenye mahitaji ya bidhaa hizo.

Alitaja Afrika Kusini kuwa miongoni mwa masoko ambayo Tanzania tayari inapeleka baadhi ya mazao yake, yakiwamo ndizi na parachichi, akisema uwepo wa wadau kutoka nchi hiyo ni fursa ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kutafuta wanunuzi wapya.

Mkindi alisema kuongeza uzalishaji bila kuwa na masoko ya uhakika hakuwezi kuleta manufaa yanayotarajiwa kwa wakulima, hivyo jukwaa hilo linalenga kuunganisha pande zote za mnyororo wa thamani.

Alisema mbali na masoko, jukwaa hilo litatoa nafasi kwa wakulima kujifunza na kupata teknolojia mpya zitakazoongeza tija katika uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa mazao.

Alisema teknolojia hizo zinatoka ndani na nje ya Afrika, hivyo wakulima watapata fursa ya kukutana moja kwa moja na wazalishaji na wauzaji wake ili kujifunza suluhisho zinazoweza kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza ushindani katika masoko.

“Wakulima wetu wanahitaji teknolojia kuanzia kwenye uzalishaji mpaka kwenye uhifadhi na usafirishaji wa mazao. Watakaposhiriki kwenye maonyesho haya watapata fursa ya kukutana na wazalishaji na wauzaji wa teknolojia mbalimbali zitakazowaongezea tija,” alisema.

Alisema TAHA inafanya kazi na wakulima zaidi ya 40,000 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, Unguja na Pemba, kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha uzalishaji na kuwaunganisha na masoko.

Kwa upande wake, Makalla aliongeza ujio wa wageni hao pia ni fursa ya kuitangaza Arusha kama kitovu cha utalii, akiwataka wadau wa sekta hiyo kutumia jukwaa hilo kutangaza vivutio vilivyopo mkoani humo.

Alisema wageni hawapaswi kuishia kushiriki maonyesho na mikutano ya biashara pekee, bali wanapaswa kupata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii ili wawe mabalozi wa Tanzania katika nchi zao na uwezekano wa kurejea kama watalii.

“Arusha ni kitovu cha utalii. Hawa wageni hawatakuja kwa ajili ya maonyesho pekee, bali tunataka wapate nafasi ya kuona vivutio vyetu, kuitangaza Arusha na hatimaye kurudi kama watalii,” alisema.

Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.


Ends.


Post a Comment

أحدث أقدم