TUMAINI SENIOR YATAKA KUONGEZA UDAHILI, YAHITIMISHA MIAKA 10
Na Joseph Ngilisho | MAKUYUNI-MONDULI
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa shule hiyo, Martin Msengi, wakati wa mahafali ya nane ya Kidato cha Sita yaliyohitimishwa na wanafunzi 43, sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya shule hiyo.
Msengi alisema shule imeendelea kupiga hatua katika kuboresha huduma za elimu, ikiwamo kuanzisha mkondo mpya wa masomo ya TEHAMA, hatua inayolenga kuongeza fursa za kielimu kwa wanafunzi.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, shule inakabiliwa na changamoto ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na mikondo mbalimbali ya masomo, hivyo inaangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya wanafunzi watakaopokelewa mwaka ujao.
Alisema, “Tunaangalia namna gani mwakani tunaweza kupokea kundi la pili la wanafunzi ili kukidhi hitaji hilo.”
Akizungumzia mafanikio ya shule hiyo katika kipindi cha miaka 10, Msengi alisema yamechangiwa na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa elimu, uongozi wa shule, bodi ya wakurugenzi, mashirika yanayofadhili elimu pamoja na jamii inayozunguka shule hiyo.
Aliwataja wazazi kuwa miongoni mwa wadau muhimu waliochangia maendeleo ya shule, akisema wamekuwa wakiiamini taasisi hiyo kwa kuwapatia watoto wao elimu na kuiwezesha kujiendesha kupitia ada.
Alisema wazazi wamekuwa sehemu muhimu ya safari ya mafanikio ya shule hiyo, akiwashukuru kwa kuendelea kushirikiana na uongozi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu katika mazingira yanayofaa.
Mkuu huyo wa shule pia alitoa shukrani kwa uongozi wa shule za Tumaini, akiwataja Mkurugenzi Sam Modesty Bayo, menejimenti na bodi ya wakurugenzi kwa ushirikiano wao katika kusimamia maendeleo ya taasisi hiyo.
Aidha, alishukuru mashirika mbalimbali yanayosaidia watoto kupata elimu pamoja na jamii inayozunguka shule hiyo kwa mchango wao katika kufanikisha safari ya miaka 10.
Katika hatua nyingine, aliwapongeza wazazi wa wanafunzi 43 waliohitimu Kidato cha Sita kwa ushirikiano wao na imani waliyoendelea kuionyesha kwa shule hiyo hadi kufikia hatua ya mahafali hayo.
Msengi alihitimisha hotuba yake kwa kumshukuru mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko wa kushiriki mahafali hayo na maadhimisho ya miaka 10 ya shule, akisema ushiriki wake ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kukuza elimu.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya kutathmini safari ya shule hiyo tangu ilipoanzishwa miaka 10 iliyopita, pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza ubora wa elimu na kupanua fursa kwa wanafunzi.
Ends































إرسال تعليق