SERIKALI KUREJESHA MASHAMBA YA MAUA ARUSHA, KULENGA SOKO LA DUNIA
....Asema miundombinu ya mashamba yaliyokuwa yakizalisha maua kwa ajili ya kuuza nje isiachwe ipotee, ataka wawekezaji kurejesha uzalishaji wa roses; ataja upotevu wa mazao ya bustani kuwa changamoto kubwa, asisitiza vijana na wanawake kunufaika na fursa za kilimo
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imetakiwa kurejesha katika uzalishaji mashamba ya maua yaliyokuwa yakizalisha maua ya waridi (roses) kwa ajili ya masoko ya kimataifa mkoani Arusha, baada ya baadhi ya maeneo hayo kugeuzwa kuwa Pmakazi na kusahaulika kwa miundombinu iliyokuwepo ya kilimo cha maua.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi,Nov 9,2026 wakati akifungua Jukwaa la Kimataifa la HortiLogistica Africa katika viwanja vya TGT, nje kidogo ya Jiji la Arusha, ambako amesisitiza kuwa Tanzania haiwezi kuongeza ushindani katika soko la kimataifa la mazao ya bustani bila kutumia ipasavyo miundombinu na fursa zilizopo nchini.Alisema ingawa ukuaji wa miji na upatikanaji wa maeneo ya makazi ni muhimu, Serikali inapaswa kuhakikisha mashamba yaliyobaki yanarejeshwa katika shughuli za kilimo ili Tanzania irejee kuzalisha na kuuza maua katika masoko ya kimataifa.
Alisema: “Leo hii ukiuliza tuna-export roses? Unaweza kukuta hatu-export hata rose moja. Kuna mashamba yale ambayo yalirudishwa serikalini na yalikuwa na miundombinu ya kuzalisha roses kwa ajili ya soko la kimataifa. Kila siku mazao yalikuwa yanaondoka hapa.”
Aliongeza kuwa Tanzania ilikuwa na uwezo wa kuzalisha maua yaliyokuwa yakihitajika katika masoko ya nje, lakini kushindwa kutumia miundombinu iliyokuwepo kumechangia kupoteza fursa hiyo, huku nchi jirani zikiendelea kufanya vizuri katika biashara ya maua.“Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, yale mashamba yaliyobaki yarejee kufanya kazi iliyokuwa inafanyika hapo awali. Hili turudi kuzalisha roses ambazo zilikuwa zinahitajika katika soko la kimataifa. Tutaona hata export yetu itaongezeka,” alisema.
Ndejembi alisema kurejeshwa kwa mashamba hayo kutafungua fursa kwa vijana wa Arusha na wawekezaji wengine kushiriki katika uzalishaji wa maua, kuongeza ajira na kutumia jukwaa la HortiLogistica Africa kuunganisha wazalishaji na wanunuzi wa kimataifa.
Alisema Tanzania inapaswa kuacha mtazamo wa kutegemea masoko ya Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati pekee, badala yake itumie pia fursa za soko la kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais alisema pamoja na Tanzania kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya bustani, bado kuna changamoto ya upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, hali inayopunguza mapato ya wakulima na kudhoofisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko.
Alitolea mfano wa mananasi yanayozalishwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro, akisema baadhi ya mazao hayo huoza mashambani au pembezoni mwa barabara kwa kukosa masoko na mifumo bora ya kuyakusanya, kuyahifadhi na kuyasafirisha.
Alisema hali kama hiyo pia inajitokeza katika uzalishaji wa parachichi mkoani Njombe, Mbeya, Manyara na maeneo mengine, ambako wakulima wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya uzalishaji lakini wanakosa mifumo madhubuti ya kuhakikisha mazao yao yanafika kwa walaji yakiwa katika ubora unaotakiwa.
“Tunazalisha sana, wakulima wetu wanajitoa sana lakini tunapoteza zao lile ambalo tunazalisha. Mananasi yanazalishwa mengi, lakini ukisimama njiani unakuta mengine yanaoza. Tuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika vituo vya kukusanyia mazao, maghala, teknolojia za kisasa za kuhifadhi na miundombinu ya mnyororo wa baridi (cold chain) ili kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya mazao.
Akizungumzia mafanikio ya sekta ya bustani, Ndejembi alisema Tanzania imepiga hatua katika uzalishaji wa parachichi, maarufu kama dhahabu ya kijani, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 149,340 mwaka 2023 hadi tani 203,473 mwaka 2026, sawa na ongezeko la takribani asilimia 36.
Alisema mauzo ya parachichi nje ya nchi yamefikia thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 255, mafanikio aliyoyahusisha na jitihada za Serikali, ikiwamo ruzuku ya miche kwa wakulima.
Hata hivyo, alisema mafanikio hayo yanapaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi kwa kuhakikisha miche inayotolewa kwa ruzuku inawafikia walengwa na inazalisha matunda yanayokidhi viwango na mahitaji ya masoko.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya miche 130,000 kwa mwaka, lakini kuna umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha wakulima wanapata teknolojia, utaalamu na masoko kabla ya kuwekeza katika uzalishaji.
Alitoa mfano wa kijana aliyefanikiwa kupata soko la nje kupitia ushirikiano na Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA), na kuanza kuzalisha kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na wanunuzi wa kimataifa.
Alisema mfano huo unaonesha umuhimu wa Serikali kutofanya kazi peke yake, bali kushirikiana na sekta binafsi ili kuunganisha wakulima na masoko tangu mwanzo wa uzalishaji.
Makamu wa Rais alisema sekta ya mazao ya bustani nchini inakua kwa wastani wa asilimia tisa hadi 12 kwa mwaka, huku uzalishaji ukiongezeka kutoka tani milioni 8.4 mwaka 2023 hadi tani milioni 9.7 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 15.9.
Alisema thamani ya mauzo ya nje ya mazao hayo ilifikia dola za Marekani milioni 569 mwaka 2024, kutoka milioni 290.7 mwaka 2020, hatua inayoonesha nafasi kubwa ya sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuongeza kipato cha wakulima.
Alisema thamani ya uagizaji wa matunda na mboga duniani ilifikia takribani dola bilioni 379.45 mwaka 2024, huku Marekani, Ujerumani, China, Uholanzi na Uingereza zikiwa miongoni mwa masoko makubwa.
Alisema Kenya, Ethiopia na Rwanda zimeonesha ushiriki mzuri katika biashara ya mazao ya bustani duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuimarisha uzalishaji, teknolojia, ubora na mifumo ya masoko ili kushindana na nchi hizo.
WAWEKEZAJI KUITWA KUCHANGAMKIA FURSA
Ndejembi alisema Tanzania imejaliwa ardhi yenye rutuba, vyanzo vya maji na hali mbalimbali za kiikolojia zinazowezesha uzalishaji wa mazao ya bustani kwa nyakati tofauti za mwaka.
Alisema mazao yenye fursa kubwa ni pamoja na parachichi, maembe, machungwa, mananasi, ndizi, mboga mbalimbali, maua na viungo, ambayo yanaweza kuhudumia masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Aliwaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika uzalishaji, usindikaji, upatikanaji wa pembejeo bora, teknolojia, vituo vya ukusanyaji wa mazao, maghala, huduma za uthibitishaji ubora na usalama wa chakula pamoja na usafirishaji.
Alisema Serikali inatambua nafasi ya sekta binafsi katika kukuza kilimo cha kisasa na chenye tija, akikipongeza Chama cha TAHA kwa mchango wake katika kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani nchini.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, wakulima na wawekezaji ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania haibaki kuwa nchi inayozalisha mazao mengi bila kuyauza kwa thamani inayostahili.
Ends



إرسال تعليق