SERIKALI KUBORESHA MAKAZI YA BABA ALIYEFIWA NA MWANAE AJALI YA LORI
...Msumi aahidi kugharamia matibabu ya Pius Musa, aliyeshindwa kutoka kitandani kuaga mwili wa mwanaye Catherine
Na Joseph Ngilisho | Arumeru
SERIKALI imeahidi kuboresha makazi ya familia ya Pius Musa, baba wa Catherine Pius, mmoja wa wanafunzi watatu waliofariki dunia katika ajali ya lori wilayani Arumeru, pamoja na kugharamia matibabu yake kutokana na hali yake ya kiafya.Tukio lililogusa hisia za waombolezaji ni pale jeneza lililokuwa na mwili wa Catherine lilipopelekwa hadi chumbani kwa baba yake, Pius Musa, ambaye kutokana na hali yake ya kiafya alilazimika kubaki kitandani huku akiaga mwili wa mwanaye kwa uchungu mkubwa bila kuinuka kitandani.
Akizungumza na familia hiyo, Msumi alisema Serikali imeguswa na msiba huo, lakini pia na hali ya kiafya ya Pius ambaye anahitaji matibabu, akiahidi kuwa gharama zote za matibabu zitashughulikiwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau.
Alisema baada ya shughuli za mazishi, Serikali itazungumza na familia hiyo ili kupanga namna ya kumfikisha Pius hospitalini kwa ajili ya kuanza matibabu.
“Pamoja na kuhakikisha tunawapumzisha watoto wetu hawa katika safari yao ya mwisho, jukumu letu jingine ni kuhakikisha baba Catherine anapata matibabu anayohitaji. Serikali itashughulikia gharama za matibabu yake,” alisema Msumi.
Aliongeza kuwa Serikali haitaiishia katika matibabu pekee, bali itashirikiana na wadau kuboresha makazi ya familia hiyo ili wazazi hao waishi katika mazingira bora.
“Baba Catherine na mama Catherine, haya makazi tutayabadilisha na kuyaboresha tofauti na hali yalivyo sasa. Sisi kama Serikali, kwa kushirikiana na wadau, tupo pamoja nanyi katika kipindi hiki,” alisema.
Akizungumzia marehemu Catherine, Msumi alisema alikuwa mwanafunzi mwenye nidhamu, bidii na aliyefanya vizuri katika masomo yake, huku akiwa msaada mkubwa kwa wazazi wake.
Alisema Serikali itaendelea kuwa karibu na familia hiyo kuhakikisha inapata msaada unaohitajika, ikiwemo matibabu ya Pius na uboreshaji wa makazi yao.

Post a Comment