Ad
Breaking🔥

CRDB YAMWAGA MADAWATI KANDA YA KASKAZINI, NAMANGA YANUFAIKA, DC KALI AIPONGEZA AOMBA TENA!

CRDB YAKABIDHI MADAWATI 50 NAMANGA, DC KALI AIPONGEZA AOMBA TENA!

...Wanafunzi 150 wanufaika, Kalli aitaka benki hiyo kuongeza mengine 50, shule ilikuwa na upungufu wa madawati 200

Na Joseph Ngilisho |LONGIDO 

BENKI ya CRDB imekabidhi madawati 50 katika Shule ya Msingi Namanga, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, yatakayowanufaisha wanafunzi 150, huku Mkuu wa Wilaya hiyo, Salumu Kalli, akiitumia fursa hiyo kuiomba benki hiyo kuongeza madawati mengine 50 ili kupunguza zaidi uhaba wa samani za shule.

Madawati hayo yametolewa kupitia kampeni ya benki hiyo ya Keti Tujifunze, inayolenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kupata elimu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Kalli alisema msaada huo umeondoa sehemu ya changamoto iliyokuwa ikiikabili shule hiyo, akieleza kuwa madawati yaliyokabidhiwa yatawapa wanafunzi 150 nafasi ya kukaa na kujifunza katika mazingira bora.

Alisema mchango huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutatua changamoto zinazokabili jamii, hususan katika sekta ya elimu.


“Madawati haya ambayo tumeyakalia ni kielelezo kwamba CRDB inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha miundombinu ya elimu. Madawati haya 50 hatukuwa nayo, lakini CRDB wakaona hapana, twende tukayapeleke,” alisema Kalli.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya hakusita kuwasilisha ombi jingine kwa benki hiyo, akisema mahitaji ya shule hiyo bado ni makubwa na kwamba msaada uliotolewa unapaswa kuwa chachu ya kuendelea kushirikiana.

“Tunapowashukuru tunawaomba tena. Ninavyoifahamu CRDB, naamini mnaweza kuongeza zaidi. Kwa hiyo, pamoja na maneno mazuri yaliyosemwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini, naomba mrudi kuongeza madawati mengine 50 ili tumalize changamoto hapa,” alisema.

Alisema ombi hilo limezingatia hali halisi ya mahitaji ya shule hiyo, huku akieleza kuwa ushiriki wa wadau kama CRDB ni muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za elimu.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, alisema msaada huo ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

Alisema CRDB inaunga mkono sera na juhudi za Serikali za kuimarisha elimu nchini, ndiyo maana imeanzisha kampeni ya Keti Tujifunze inayolenga kuchangia upatikanaji wa madawati na kuboresha mazingira ya shule.

Sadat alieleza kuwa benki hiyo haitajikita Namanga pekee, bali imepanga kusambaza madawati katika shule mbalimbali za Kanda ya Kaskazini kwa muda wa wiki nzima, hatua inayolenga kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji.

Alisema mpango huo unaendana na kaulimbiu ya benki hiyo ya Ulipo Nipo, inayosisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kuwa karibu na jamii na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Namanga, Debora, aliishukuru CRDB kwa msaada huo, akisema kabla ya kupokea madawati hayo shule ilikuwa na upungufu wa madawati 200.

Alisema kupatikana kwa madawati hayo 50 kumepunguza changamoto iliyokuwepo na kuboresha mazingira ya wanafunzi kusoma, huku akieleza kuwa bado juhudi zaidi zinahitajika ili kukamilisha mahitaji ya shule hiyo.

Msaada huo unakuja wakati Serikali ikiendelea kuhimiza ushiriki wa wadau mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo madarasa, madawati na vifaa vingine muhimu vinavyowezesha wanafunzi kujifunza katika mazingira bora.







Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post