MACKENZIE AHUKUMIWA MIAKA 200 JELA KWA MAUAJI YA SHAKAHOLA
By ArushaDigital-KENYA
Mahakama Kuu ya Mombasa nchini Kenya imemhukumu mhubiri Paul Nthenge Mackenzie kifungo cha miaka 200 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na vifo vya watu 191, wakiwemo watoto 190 na mtu mzima mmoja, katika mauaji ya kutisha ya Shakahola.Adhabu hiyo imetolewa leo, Novemba 6, 2026, na Jaji Diana Kavedza Mochache, baada ya Mackenzie kutiwa hatiani Oktoba 19, 2026, pamoja na washtakiwa wenzake 28 katika kesi iliyotikisa Kenya na kuvuta hisia za kimataifa.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mackenzie amehukumiwa miaka 100 jela kwa vifo vilivyosababishwa na kuwanyima waumini wake chakula na miaka mingine 100 kwa mauaji ya moja kwa moja. Adhabu hizo zinatakiwa kutumikishwa mfululizo, badala ya kutumikishwa kwa wakati mmoja.
Uchunguzi wa kesi hiyo ulibaini kuwa Mackenzie aliwashawishi na kuwaelekeza wafuasi wake kufunga kula hadi kufa, akiwahadaa kuwa kufanya hivyo kungewasaidia kukutana na Yesu.
Tukio hilo lilifichuka mwaka 2023, baada ya mamlaka za Kenya kuanza kufukua miili ya mamia ya watu kutoka katika makaburi ya kina kifupi yaliyokuwa ndani ya Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, katika tukio lililoibua mjadala mkubwa kuhusu udhibiti wa shughuli za kidini na usalama wa waumini.
#ArushaDigitalUpdates
Post a Comment