Ad
Breaking🔥

LUKUMAY: KANISA LIJENGE WATOTO KATIKA IMANI, MAADILI,AWAZAWADIA 500,000 WATOTO WA KIPA IMARA

LUKUMAY: KANISA LIJENGE WATOTO KATIKA IMANI, MAADILI

...Ataka vijana wakue wakimtambua Mungu, atoa Sh500,000 kuwaunga mkono watoto wawili wa diwani waliohitimu Kipaimara

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, amesisitiza umuhimu wa kanisa na familia kushirikiana katika malezi ya watoto kwa kuwajenga kiroho na kimwili ili wakue katika misingi ya imani, maadili mema na kumtambua Mwenyezi Mungu.

Lukumay alitoa kauli hiyo jumapili Nov 15,2026 wakati wa hafla ya chakula iliyoandaliwa kusherehekea hatua muhimu ya watoto wawili wa diwani wa jimbo hilo, Faraja, waliopokea Sakramenti ya Kipaimara, ambayo ni moja ya hatua muhimu katika safari ya imani ya Kikristo.

Alisema Kipaimara si tukio la sherehe pekee, bali ni hatua muhimu inayopaswa kwenda sambamba na malezi endelevu ya kiroho ili watoto waendelee kuimarika katika imani na kutambua wajibu wao kwa Mungu na jamii.

Alieleza kuwa mafundisho ya dini tangu utotoni yana mchango mkubwa katika kujenga kizazi chenye hofu ya Mungu, nidhamu na misingi imara ya maisha.




Akizungumzia safari yake ya maisha, Lukumay alisema imani na kumcha Mungu vimekuwa nguzo muhimu katika mafanikio yake, akirejea kipindi alipokuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Elboru, ambako alikutana na ujumbe uliosomeka, “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa.”

Alisema ujumbe huo ulimjengea mtazamo wa kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yake na kwamba mafanikio aliyoyapata, ikiwamo kuwa mbunge, yanatokana na neema ya Mwenyezi Mungu.

“Ninamshukuru Mungu kwa mambo mengi aliyotenda katika maisha yangu. Hata katika safari ya ubunge, viongozi wa kanisa, madiwani na wananchi waliniombea. Maombi yenu yamekuwa sehemu muhimu ya safari yangu,” alisema.

Katika hotuba yake, Lukumay pia alilitaka kanisa kuendelea kuliombea Taifa ili amani na utulivu viendelee kudumu, akisema mazingira hayo ndiyo yanayowawezesha Watanzania kuishi kwa umoja na kushiriki shughuli za maendeleo.

Alisisitiza umuhimu wa kuliombea Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe afya njema, hekima na nguvu za kuendelea kuliongoza Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Wajibu wa kanisa ni pamoja na kuliombea Taifa letu. Bila amani tusingekuwa hapa leo tukisherehekea. Tuendelee pia kuiombea Serikali yetu ili iendelee kutuletea maendeleo,” alisema.

Mbunge huyo alimpongeza diwani Faraja na familia yake kwa kuhakikisha watoto wanapata malezi yanayozingatia misingi ya dini, akisema hatua hiyo ni uwekezaji muhimu katika maisha yao ya sasa na baadaye.

Katika kuunga mkono sherehe hiyo, Lukumay alikabidhi Sh500,000 kwa ajili ya vijana hao, akieleza kuwa fedha hizo zitasaidia mahitaji yao katika hafla hiyo.

Alisema anathamini juhudi za wazazi na walezi wanaowapeleka watoto katika mafundisho ya dini na kuhakikisha wanakua katika misingi inayomjenga mtu kiroho na kijamii.

Alimalizia kwa kuwaombea watoto hao waendelee kukua katika imani, wakimtambua Mungu na kuishi kwa kuzingatia mafundisho ya Kikristo.









Ends

Post a Comment

أحدث أقدم