LUKUMAY ATOA WITO WA KUJENGA WATOTO KIROHO, ACHANGIA MILIONI 1 KANISANI
Asema malezi ya kiimani ni msingi wa kuwajenga watoto kuwa raia wema na viongozi bora wa baadaye
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, ametoa wito kwa wazazi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kushirikiana katika malezi ya watoto kwa kuwajenga katika misingi imara ya imani, maadili mema na kumcha Mungu ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha.
Aidha, mbunge huyo amechangia Sh milioni moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Tarajali Oltrumet, Mtaa wa Oltrumet.
Hata hivyo kanisa hilo kupitia kiongozi wa ibada hiyo ya Kipaimara , Mch.Solomon Dereva ,Msaidizi wa mkuu wa jimbo ,lilimpongeza Mbunge Lukumay kwa kuwa mstari wa mbele kwa majitoleo yake ambayo amekuwa akiyafanya katika kusaidia jamii .
Lukumay alisema malezi ya watoto hayaishii katika kuwapatia mahitaji ya kimwili pekee, bali yanapaswa kuambatana na malezi ya kiroho yatakayowasaidia kumjua Kristo, kumwamini Mungu na kuishi kwa kufuata maadili mema.
Alisema lengo la Kipaimara si kutimiza taratibu za kidini pekee, bali ni kuwajenga watoto katika imani ya Kristo, kuwaimarisha kiroho na kimwili na kuwasaidia kufanya maamuzi yanayozingatia misingi ya Mungu katika maisha yao.
"Jambo kubwa ni kuwaimarisha na kuwajenga watoto katika imani ya Kristo, tuweze kuwasaidia na kuwafanya imara katika maisha yao ya kiroho na kimwili, lakini pia kuwafanya wamwamini Kristo tangu wakiwa katika umri mdogo," alisema.
Dkt Lukumay alisema jamii ina wajibu wa kuwaombea watoto na kuwapa mwongozo unaofaa, akibainisha kuwa malezi yanayozingatia maombi na kumtegemea Mungu yana nafasi kubwa katika kuwajenga watoto kufuata njia njema.
Alisisitiza pia umuhimu wa waumini kushiriki kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji, akisema utoaji wa misaada kwa moyo wa upendo na bila kutarajia malipo ni sehemu ya kutekeleza wajibu wa Kikristo.
Alisema kuna watoto wanaohitaji msaada wa kijamii na kiuchumi ili waweze kupata fursa za kukua na kutimiza malengo yao, hivyo akawataka wenye uwezo kutumia baraka walizonazo kuwainua wengine.
"Unapowasaidia watoto na kutoa kwa moyo wa dhati, bila kutegemea utapata nini, unakuwa umetenda jambo jema. Tuwasaidie hasa wale wanaohitaji, wakiwemo watoto wanaotoka katika familia maskini," alisema.
Mchango huo unalenga kuunga mkono juhudi za kanisa katika kutekeleza majukumu yake ya kiroho na kijamii, yakiwemo malezi ya watoto na kuwajenga waumini katika misingi ya imani na maadili mema.
Aidha, mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuhimiza waumini kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani na utulivu, akisema amani ni msingi muhimu wa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Alisema bila amani, shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo haziwezi kutekelezwa kwa ufanisi, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuiombea nchi na kudumisha mshikamano.
Pia alihimiza waumini kuwaombea viongozi wa Serikali, hususan Rais, ili Mungu awape hekima, busara na nguvu za kuongoza Taifa kwa uadilifu na kusimamia maendeleo yanayowanufaisha wananchi.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na jamii ni muhimu katika kujenga Taifa lenye maadili, mshikamano na mazingira bora kwa ajili ya ukuaji wa kizazi cha sasa na kijacho.
Dkt Lukumay alihitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la kuwajenga watoto si la wazazi pekee, bali ni la jamii nzima, akiwataka waumini kuendeleza upendo, kusaidiana na kuwaombea watoto ili wakue katika misingi imara ya kiimani na maadili.
Ends

















إرسال تعليق