LUKUMAY ATOA NASAA NZITO KWA BINTI WA ASKOFU MOLLEL,AMKABIDHI ZAWADI MIL 1
..Asema ndoa hudumu kwa heshima, uvumilivu na kutunza siri za familia, atoa Sh milioni moja kusaidia sherehe
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, ametoa nasaha kwa Lucy Godson, mtoto wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Askofu Godson Abel Mollel, akimtaka kuilinda ndoa yake kwa kuheshimu mume, kutunza siri za familia na kuzingatia uvumilivu.Dkt Lukumay alitoa nasaha hizo Nov 05,2026 wakati wa sherehe ya Send-off ya Lucy, akisema ndoa ni taasisi inayohitaji heshima, staha na uvumilivu ili iweze kudumu, huku akisisitiza kuwa mali na vitu vya thamani si msingi pekee wa maisha ya ndoa.
Alisema Lucy amepata malezi na mafunzo kutoka kwa wazazi wake pamoja na viongozi wa dini, akiwamo Askofu Mollel na viongozi wengine wa Kanisa, jambo lililomjenga hadi kufikia hatua hiyo muhimu ya maisha.
Akitoa mambo matatu ya kuzingatia katika maisha ya ndoa, Dkt Lukumay alisema jambo la kwanza ni kuheshimu ndoa na mume wake, akimtaka kutambua kuwa anaanza maisha mapya yanayohitaji kujitolea na kuheshimiana.
Pili, alimtaka kutunza siri za ndani za familia na ndoa yake, ikiwamo mambo binafsi ya mume wake, akionya dhidi ya tabia ya kupeleka mambo ya ndani ya ndoa kwa watu wengine.
Tatu, alisisitiza umuhimu wa kumwombea mume wake ili Mungu amlinde, akisema maisha ya ndoa yanahitaji kumtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na kujenga misingi imara ya upendo na uvumilivu.
“Ndoa inahitaji heshima, staha na uvumilivu. Mali na vitu mbalimbali vipo, lakini hayo ndiyo yatakayosaidia ndoa yenu kudumu,” alisema Dkt Lukumay.
Alikabidhi fedha hizo kwa Askofu Mollel na kumwomba amsaidie Lucy kupata ndafu kwa ajili ya sherehe hiyo.
Sherehe hiyo imevuta mamia ya wananchi,waumini wa Kanisa hilo,Maaskofu,wachungaji,viongozi mbalimbali wa dini,viongizi wa serikali na wanasiasa
Ends






إرسال تعليق