Ad
Breaking🔥

KADOGOSA AMKALIA KOONI MKANDARASI ARUSHA, ATOA ONYO KALI

KADOGOSA AMKALIA KOONI MKANDARASI ARUSHA, ATOA ONYO KALI 

Agoma kuondoka kwa vifaa baada ya kulipwa fedha za maandalizi ya ujenzi, ataka vifaa vilivyokosekana vifike kabla ya Ijumaa na kuonya kuhusu kubadilisha wataalamu mara kwa mara.

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kungu Kadogosa, amemkalia kooni mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini–Timbolo wilayani Arumeru, akimtaka kuacha tabia ya kuondoa vifaa baada ya kulipwa fedha za maandalizi ya ujenzi (mobilization), akisema vitendo hivyo vinachelewesha utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Kadogosa alisema Serikali haitakubali mkandarasi kulipwa fedha kwa ajili ya kujiandaa kutekeleza mradi, kisha kuleta vifaa eneo la kazi na baadaye kuviondoa bila sababu za msingi, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka masharti ya mikataba.


Alisema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi katika Kata ya Kimnyaki wilaya ya Arumeru kunakotekelezwa mradi wa barabara ya Mianzini- Timbolo hadi Ngaramtoni , ambapo alikutana na changamoto mbalimbali za utekelezaji na kutoa maelekezo kwa meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, mkandarasi pamoja na washauri elekezi.

“Mkandarasi tunampa fedha kwa ajili ya kufanya mobilization, anakuja kuleta vifaa halafu anaviondoa. Hiyo sitaki kuisikia wala kuiona tena. Kama jambo hilo limetokea, tunachora mstari kuanzia hapa kwenda mbele. Hatutaki liendelee kujirudia,” alisema Kadogosa.

Alisema haikubaliki kwa mkandarasi kuondoa vifaa vya ujenzi bila usimamizi na uelewa wa wahusika wanaosimamia mradi, akiwataka TANROADS kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji inafuatiliwa kwa karibu ili kuzuia uzembe na ucheleweshaji.

Kadogosa pia alikemea tabia ya kutoa maelezo yasiyoeleweka kuhusu changamoto za mradi, akisisitiza kuwa watendaji wanapaswa kueleza ukweli badala ya kutoa sababu zisizo na msingi wanapoulizwa kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema TANROADS ndiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya kiufundi na miundombinu ya barabara, ikiwamo madaraja, hivyo haipaswi kukwepa wajibu wake kwa kutoa maelezo yanayoonyesha kutokuwa na taarifa kuhusu kinachoendelea kwenye mradi.

"Tuache hizi ngonjera. Kama kuna kosa limefanyika, semeni wazi kwamba hapa tumekosea kwa sababu hizi. Mimi ni binadamu kama ninyi, lakini tusianze kudanganyana kwa sababu hilo ni tatizo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alimtaka mkandarasi kuhakikisha kifaa cha Chip Spreader kinachohitajika katika hatua za ujenzi kinafikishwa eneo la mradi kabla ya Ijumaa, akimtaka meneja wa TANROADS kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha mkandarasi anawasilisha uthibitisho kwa maandishi.

Kadogosa alisema mkandarasi anapaswa kuzingatia mpango wa utekelezaji wa mradi na kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika vinapatikana kwa wakati ili kazi iendelee bila kusimama.

Aidha, alimuonya mkandarasi dhidi ya tabia ya kubadilisha wataalamu mara kwa mara katika eneo la mradi, akisema hali hiyo inasababisha kupoteza mwendelezo wa kazi kwa kuwa kila mtaalamu mpya anahitaji muda wa kujifunza na kuelewa mradi.

“Msibadilishe wafanyakazi kila wakati. Kila unapomleta mtu mpya hapa, anaanza kujifunza upya, jambo ambalo linachelewesha kazi. Tunataka mradi ukamilike haraka iwezekanavyo,” alisema.

Akizungumza na wananchi wa Kimnyaki, Kadogosa alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ndani ya muda mfupi, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini.

Alisema ziara yake imelenga kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Nimekuja leo, lakini mtaniona tena. Tumekubaliana kwamba kufikia Ijumaa vifaa vilivyokosekana vitakuwa vimefikishwa hapa ili ujenzi uendelee. Nitahitaji taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo,” alisema.

Kadogosa aliongeza kuwa Serikali haitavumilia malalamiko ya mara kwa mara kuhusu kuharibika kwa vifaa vya ujenzi, akiwataka TANROADS na washauri elekezi kuhakikisha vifaa vinavyopokelewa kutoka kwa wakandarasi vinakaguliwa kwa umakini na kuthibitishwa kuwa vinafanya kazi ipasavyo.

Alisema kama mkandarasi ana changamoto ya vipuri, anapaswa kuchukua hatua za haraka kuzitatua badala ya kuruhusu vifaa kusimama na kuathiri kasi ya mradi.

Waziri huyo alisema usimamizi madhubuti wa mikataba ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya barabara inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, huku akisisitiza kuwa jukumu la TANROADS ni kuhakikisha wakandarasi wanatekeleza wajibu wao kikamilifu.


Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post