Ad
Breaking🔥

CHITINKA AIPA TANO PCCB SACCOS, ATOA WITO KWA SACCOS ZATAJWA KUWA NGUZO YA UCHUMI IMARA KWA WATUMISHI

SACCOS ZATAJWA KUWA NGUZO YA UCHUMI IMARA KWA WATUMISHI

...Mrajis Dodoma aipongeza PCCB SACCOS kwa mtaji mkubwa na kufanya vizuri nchini, ataka watumishi zaidi kujiunga

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

VYAMA vya kuweka na kukopa (SACCOS) vimetajwa kuwa chombo muhimu katika kuboresha maisha ya watumishi kwa kuwawezesha kuweka akiba, kupata mikopo na kujenga ustawi wa kiuchumi kupitia mfumo wa ushirika.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, alisema SACCOS zina nafasi kubwa katika kuwawezesha watumishi kujikwamua kiuchumi, akiwataka kuongeza ushiriki wao katika vyama hivyo na kuzingatia nidhamu ya mikopo.

Chitinka alitoa kauli hiyo Nov 16,2026 jijini Arusha wakati wa Mkutano Mkuu 23 wa Mwaka wa PCCB SACCOS, ambapo pia alikipongeza chama hicho kwa kukua kwake kiuchumi, kuwa na mtaji mkubwa na kufanya vizuri katika sekta ya ushirika nchini.

Alisema PCCB SACCOS ni miongoni mwa vyama vinavyoonesha mafanikio katika uendeshaji wa shughuli zake, akieleza kuwa maendeleo hayo yanapaswa kuwa chachu kwa vyama vingine na wanachama kuendelea kuimarisha ushiriki wao katika kujenga uchumi wa pamoja.

Alisema mkutano mkuu ni chombo muhimu zaidi cha wanachama kufanya maamuzi kuhusu uendeshaji na maendeleo ya chama, ikiwemo kujadili na kupitisha bajeti, kutathmini mafanikio, kubainisha changamoto na kupanga mikakati ya mwaka mwingine wa fedha wa 2027.

Alisema SACCOS zimeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kujenga maisha bora kwa wananchi na watumishi kupitia utaratibu wa kuweka fedha na kukopa kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo ya ushirika.

"Katika SACCOS kuna taratibu nzuri zinazowaongoza wanachama kuweka akiba, kukopa na kurejesha mikopo yao. Hiki ni chombo sahihi kwa watumishi kujenga maisha yao, tofauti na baadhi ya taasisi nyingine ambazo mikopo yake inaweza kuwa na riba kubwa na kumweka mkopaji katika mazingira magumu," alisema Chitinka.

Alisisitiza kuwa SACCOS ni mali ya wanachama na wao ndio wenye mamlaka ya kufanya maamuzi kuhusu maendeleo ya vyama vyao, hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mikutano na shughuli mbalimbali za chama.

Aidha, aliwataka watumishi ambao bado hawajajiunga na vyama vya ushirika kutumia fursa hiyo kujiunga na kuongeza nguvu ya kiuchumi ya vyama hivyo.

Katika hatua nyingine, Chitinka alisisitiza umuhimu wa wanachama wanaokopa kuzingatia masharti ya mikopo na kufanya marejesho kwa wakati ili kuzuia ongezeko la mikopo chechefu.

Alisema nidhamu ya urejeshaji ni msingi wa uendelevu wa SACCOS kwa kuwa fedha zinazorejeshwa kwa wakati ndizo zinazowezesha wanachama wengine kupata mikopo, chama kujiendesha na kupata faida.

"Jambo kubwa kwa wakopaji ni kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati. Tusiruhusu mikopo chechefu, kwa sababu fedha hizo zikikwama zinawanyima nafasi wanachama wengine kukopa na kudhoofisha msingi wa ushirikiano," alisema.

Aliongeza kuwa usimamizi wa vyama hivyo utaendelea kusisitiza uzingatiaji wa sheria, taratibu na miongozo ya ushirika ili kuhakikisha SACCOS zinaendeshwa kwa uwazi na kulinda maslahi ya wanachama.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post