Ad
Breaking🔥

CRDB KUIFUNGUA KITETO KWA UZALISHAJI WENYE TIJA

CRDB, KITETO KUBADILI KILIMO NA UFUGAJI

Benki yakubali kuwezesha ufugaji wa kisasa, mikopo ya kuku kwa wanawake na kuongeza thamani ya mazao

Na Joseph Ngilisho | KITETO

WAKULIMA na wafugaji wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wanatarajiwa kunufaika na fursa mpya za uwezeshaji wa kiuchumi baada ya Benki ya CRDB kuahidi kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kupanua huduma za kifedha na kuimarisha uzalishaji katika sekta za kilimo na mifugo.

Ushirikiano huo unalenga kuleta mageuzi katika shughuli za kiuchumi za wananchi, ikiwamo kuendeleza ufugaji wa kisasa, kuwawezesha wanawake kuanzisha na kukuza miradi ya ufugaji wa kuku, pamoja na kuongeza thamani ya mazao kupitia uboreshaji wa viwanda vidogo vya usindikaji.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema, alisema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Meneja wa Kanda wa CRDB, Cosmas Sadat, yaliyolenga kuweka mikakati ya pamoja ya kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji mali na kuboresha maisha ya wananchi.

Alisema ushirikiano huo umeelekezwa katika maeneo yenye fursa kubwa za kiuchumi wilayani humo, ili kuwawezesha wakulima na wafugaji kutumia fursa zilizopo kuongeza uzalishaji, kipato na ajira.

Katika eneo la mifugo, Mwema alisema wamekubaliana kuhamasisha ufugaji wa kisasa kupitia kongani maalumu zilizotengwa na Halmashauri, zitakazokuwa chachu ya kuimarisha uzalishaji wa ng'ombe wa nyama na maziwa.

Mpango huo unalenga kuondoa changamoto za ufugaji usiozingatia tija na kuwahamasisha wafugaji kutumia mbinu bora za uzalishaji zitakazowawezesha kupata mifugo yenye ubora na kuongeza mapato yao.

WANAWAKE KUNUFAIKA NA MRADI WA KUKU


Katika hatua nyingine, ushirikiano huo umeweka msisitizo maalumu katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku kwa mfumo wa vikundi, utakaotekelezwa kupitia dirisha la Imbeju la CRDB.

Kupitia mpango huo, wanawake watapata fursa ya kuanzisha miradi ya kuku kwa utaratibu maalumu wa kukopa kuku na kurejesha mkopo kwa kulipa kwa kutumia mayai yatakayozalishwa.

Mpango huo unatarajiwa kuanza katika baadhi ya vijiji kama majaribio kabla ya uwezekano wa kupanuliwa katika maeneo mengine, ukiwa na lengo la kuwapatia wanawake chanzo endelevu cha mapato na kuimarisha uchumi wa kaya.

Utaratibu huo unaweka msisitizo katika kuwawezesha wanawake kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji badala ya kubaki watazamaji wa fursa za kiuchumi zinazowazunguka.

ALIZETI KUNUFAIKA NA VIWANDA VYA KISASA

Katika sekta ya kilimo, CRDB na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wamekubaliana kuimarisha uzalishaji wa mazao mbalimbali yanayolimwa Kiteto, sambamba na kuboresha mnyororo wa thamani ili wakulima wanufaike zaidi na mazao yao.

Moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni zao la alizeti, ambapo mpango huo unalenga kuboresha uwezo wa viwanda vidogo vya kukamua mafuta kwa kuvipatia teknolojia na mashine za kisasa.

Hatua hiyo inalenga kuongeza kiwango cha mafuta kinachokamuliwa, kupunguza upotevu wa malighafi na kuongeza ufanisi wa uzalishaji, huku ikifungua fursa zaidi za biashara na ajira katika mnyororo mzima wa zao hilo.

Uboreshaji wa viwanda hivyo pia unatarajiwa kuwasaidia wakulima kupata soko lenye tija kwa mazao yao, huku wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji wakipata nafasi ya kupanua shughuli zao.

CRDB KUUNGANA NA WILAYA KATIKA MAONESHO

Mbali na uwezeshaji wa kifedha na uzalishaji, CRDB imekubali mwaliko wa Mkuu wa Wilaya kushiriki katika matukio na maonesho mbalimbali yatakayoandaliwa Kiteto kwa lengo la kutoa elimu na ujuzi kwa wananchi.

Ushiriki huo unalenga kuongeza uelewa kuhusu fursa za kifedha, matumizi ya huduma za benki na mbinu bora za uzalishaji, ili wananchi waweze kutumia maarifa na huduma zinazopatikana kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Fadhili Alexander; Meneja wa CRDB Kiteto, Bruno Ntukey, pamoja na Meneja wa Mahusiano Serikalini wa benki hiyo, Gabriel Killian.

Ushirikiano huo unaweka msingi wa kuunganisha huduma za kifedha na uzalishaji wa moja kwa moja, hatua inayoweza kuongeza thamani ya kilimo na mifugo na kuifanya sekta hiyo kuwa injini muhimu ya uchumi wa wananchi wa Kiteto.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم