VIJANA 114 ARUSHA WAKABIDHIWA LESENI ZA UDEREVA BURE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
VIJANA 114 wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha mkoani Arusha wamekabidhiwa leseni za udereva bure baada ya kuhitimu mafunzo yaliyoratibiwa na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, kwa lengo la kuwafungulia fursa za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Akizungumza baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Arusha, ACP Zauda Mohamed, alisema mafunzo hayo yalianza na vijana 126, lakini 114 kati yao walifanikiwa kuhitimu baada ya kufaulu mitihani na kukidhi vigezo vya kupata leseni za udereva.
Alisema mpango huo unalenga kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kutumia fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji kujipatia kipato, kujitegemea kiuchumi na kuboresha maisha yao.
“Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kutumia ujuzi walioupata kujitafutia kipato na kujikwamua kiuchumi, badala ya kuendelea kukabiliwa na changamoto za maisha,” alisema.
ACP Mohamed aliwataka wahitimu hao kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, akisisitiza kuwa kupata leseni ni hatua ya kwanza, hivyo wanapaswa kuutumia ujuzi wao kwa uwajibikaji na kuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani.
Aidha, aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia watu wenye uhitaji katika jamii kwa kuwawezesha kupata ujuzi na fursa zitakazowasaidia kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake, mmoja wa wahitimu hao, Emilia Frank, aliishukuru Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwawezesha kupata mafunzo na leseni bila malipo, akisema hatua hiyo imemfungulia fursa mpya za kujipatia kipato.
Alisema leseni hiyo ni nyenzo muhimu katika kutafuta ajira au kujiajiri kupitia shughuli za udereva, huku akiahidi kutumia fursa hiyo kwa uwajibikaji na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Emilia pia alimshukuru mlezi wa programu hiyo kwa kuwaunga mkono hadi walipokamilisha mafunzo na kukabidhiwa leseni, akisema msaada huo ni hatua muhimu katika kuwasaidia vijana kujenga maisha bora.

إرسال تعليق