Ad
Breaking🔥

TANGA: WARAIBU 436 WAPOTEA KLINIKI YA METHADONE

TANGA: WARAIBU 436 WAPOTEA KLINIKI YA METHADONE

Wadau wataka ufuatiliaji uimarishwe, jamii isiwatenge waathirika

Na Hadija Bagasha | TANGA

TAKWIMU za Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo zinaonyesha kuwa waraibu 436 wa dawa za kulevya walioandikishwa kupata huduma ya Methadone wameacha kufika kliniki, hali inayoibua changamoto katika juhudi za kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kati ya waraibu 1,390 waliosajiliwa tangu huduma hiyo ilipoanzishwa mwaka 2020, ni 490 wanaoendelea kupata huduma, huku 203 wakiripotiwa kukamilisha matibabu na 102 kufariki dunia.

Hali hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa, kutoa elimu kwa jamii na kushirikisha familia katika kuwasaidia waathirika kuendelea na matibabu badala ya kuachwa bila msaada.


Akizungumzia changamoto hiyo, Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Halidy Rashid, amewataka wanaojihusisha na uingizaji na biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja, akisema vitendo hivyo vinahatarisha afya na maisha ya vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Rashid alitoa kauli hiyo Oktoba 22, 2026, wakati wa mafunzo ya kinga dhidi ya dawa za kulevya yaliyowakutanisha maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii, madaktari, walimu na makundi ya vijana.

Alisema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali, tatizo la dawa za kulevya bado linaathiri jamii, hivyo kuna haja ya kuimarisha mikakati ya kuzuia matumizi, kutambua waathirika mapema na kuwaunganisha na huduma za kitaalamu.

“Ni kweli tuna waraibu wengi ambao wameanza kupata huduma za kupona, lakini bado kuna watu wengine ambao hawajatambuliwa na wako mtaani. Jambo hili linatusikitisha sana kama halmashauri,” alisema Rashid.

Alisema nafasi ya kijiografia ya Tanga, inayopakana na nchi jirani na kuwa na mwambao wa Bahari ya Hindi, inahitaji kuimarishwa kwa udhibiti wa njia zinazoweza kutumiwa kuingiza dawa za kulevya, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi na biashara ya dawa hizo.

Rashid aliongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga inaendelea kuandaa mikakati ya kutoa elimu kuanzia ngazi za mitaa, huku akiwataka viongozi wa serikali za mitaa na kata kushirikiana na wananchi kubaini na kutoa taarifa kuhusu wanaojihusisha na biashara hiyo.

“Ninachotaka kuwaambia waingizaji wote wa dawa za kulevya kutoka nje na ndani ya nchi ni kwamba waache, kwa kuwa wanawaathiri vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya taifa,” alisema.

WARAIBU 436 WAKOSA HUDUMA

Kwa mujibu wa takwimu za huduma ya Methadone katika Hospitali ya Bombo, waraibu 436 wameacha kufika kliniki, huku juhudi za kuwatafuta na kuwahamasisha kurejea zikiendelea.

Mfamasia wa Kitengo cha Methadone katika hospitali hiyo, Fatuma Ismail, alisema kituo hicho kinashirikiana na wahudumu pamoja na asasi zinazohusika na huduma za uraibu kuwatafuta wagonjwa wanaokosa miadi yao kwa muda.

Alisema ufuatiliaji huo unalenga kuwabaini wagonjwa ambao hawajafika kliniki kwa wiki moja au mbili, kuwafikia na kuwahamasisha kurejea ili wataalamu watathmini hali zao na kuendelea kuwapatia huduma zinazofaa.

“Tunafanya orodha ya wagonjwa ambao wamepotea kwa muda, labda wiki moja au mbili. Watu wa asasi pamoja na sisi hapa tunawatafuta, tukiwapata tunawaleta kliniki na kuangalia maendeleo yao,” alisema Fatuma.

Alisema ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, familia na asasi ni muhimu katika kuwafikia wagonjwa hao na kuwasaidia kuendelea na matibabu.

METHADONE YAREJESHA MATUMAINI

Pamoja na changamoto hiyo, wataalamu wa afya wanasema huduma ya Methadone imekuwa na mchango katika kuwasaidia watu wenye uraibu wa dawa za kulevya, hususan heroini, kudhibiti utegemezi na kurejea katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Daktari wa afya ya akili na utengamao katika huduma ya MAT, Dk Ally Mapinda, alisema baadhi ya wanaopata huduma hiyo wameweza kurejea katika familia zao, kuanzisha shughuli za kujipatia kipato na kushiriki tena katika shughuli za kijamii.

Alisema baadhi yao wamerejea kazini, wengine wameanzisha familia, huku wengine wakijishughulisha na uvuvi, udereva na uendeshaji wa bodaboda.

“Tunajivunia kwa sababu wamerudi kwenye jamii, wamesaidia familia zao, wengine wameoa, wengine wamerudi makazini, na wengine ni wavuvi, madereva na waendesha bodaboda,” alisema Dk Mapinda.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya huduma hiyo yanategemea wagonjwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, kutumia dawa kwa utaratibu unaotakiwa na kuendelea na ufuatiliaji wa kitabibu.

Akizungumzia vifo vya wagonjwa 102 waliosajiliwa katika huduma hiyo, Dk Mapinda alisema haviwezi kuhusishwa moja kwa moja na Methadone pekee, kwa kuwa vinaweza kutokana na sababu mbalimbali za kiafya na mazingira ya maisha ya wagonjwa.

Alitaja matumizi ya dawa kupita kiasi, kuchanganya Methadone na vilevi vingine, pamoja na magonjwa kama shinikizo la damu, kifua kikuu na septicemia, ambayo ni hali ya maambukizi makali mwilini, kuwa miongoni mwa changamoto zinazoweza kuhatarisha afya za wagonjwa.

Pia alitaja ajali za barabarani kuwa miongoni mwa sababu zilizoripotiwa kuchangia baadhi ya vifo.

“Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni overdose, ambapo mtumiaji anatumia Methadone na kuichanganya na vilevi vingine. Kuchanganya hivyo ni hatari kiafya na kunaweza kusababisha kifo,” alisema.

Alitoa wito kwa wagonjwa kufuata maelekezo ya wataalamu na kuepuka kuchanganya dawa na vilevi vingine ili kupunguza hatari zinazoweza kuhatarisha maisha yao.

WADAU WATAKA JAMII ISIWATENGE

Kwa upande wake, Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Gift of Hope jijini Tanga, Said Bandawe, alisema wameona umuhimu wa kuandaa wakufunzi watakaotoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya na namna ya kuzuia matumizi yake katika maeneo mbalimbali ya kazi na kwenye jamii.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki kutambua hatari zinazohusiana na dawa za kulevya, kuzuia matumizi na kuwahamasisha waathirika kutafuta huduma za kitaalamu badala ya kutengwa.

Bandawe alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa kwa kutegemea Serikali na vyombo vya usalama pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wazazi, vijana, waandishi wa habari, viongozi na wananchi kwa ujumla.

“Vita dhidi ya dawa za kulevya si ya mtu mmoja, si ya mamlaka wala viongozi pekee. Ni ya kwetu sote, wazazi, vijana, waandishi wa habari na jamii nzima, ambayo inapaswa kushiriki,” alisema Bandawe.

Aliishukuru Programu ya TangaYetu, chini ya uratibu wa Halmashauri ya Jiji la Tanga na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kwa kushirikiana katika juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Kwa ujumla, takwimu za huduma ya Methadone zinaonyesha kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya, bado kuna umuhimu wa kuimarisha huduma za matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.

Changamoto ya waraibu 436 kuacha kufika kliniki ya Bombo inaweka wajibu kwa Serikali, wataalamu wa afya, familia na jamii kuhakikisha wanaohitaji msaada wanafikiwa, wanahamasishwa kurejea kliniki na wanapata fursa ya kujenga upya maisha yao.

Mwisho.

Post a Comment

أحدث أقدم