TAKUKURU WAOMBWA KUCHUNGUZA UJENZI WA GHOROFA LEVOLOSI
Wakazi wadai eneo lililotengwa kwa miundombinu ya maji taka na mvua limevamiwa, wataka kibali cha ujenzi na umiliki wa kiwanja uchunguzwe
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
UONGOZI wa Kata ya Levolosi na Mtaa wa Levolosi jijini Arusha umeiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha kuingilia kati na kuchunguza umiliki wa kiwanja namba 428 pamoja na uhalali wa kibali cha ujenzi wa jengo la biashara la ghorofa namba 235 linalojengwa katika eneo hilo.
Viongozi hao wanadai kuwa eneo hilo lilikuwa limetengwa kwa matumizi ya wazi, likiwemo kupitisha miundombinu ya maji taka na maji ya mvua, lakini kwa sasa linaendelezwa kwa ujenzi wa jengo la biashara jambo ambalo wanasema limeibua maswali kuhusu uhalali wa umiliki na taratibu zilizofuatwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi hao pamoja na baadhi ya wakazi wa kata hiyo walisema kiwanja hicho kilikuwa mali ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) miaka ya 1990, kabla ya kufutiwa hati kwa madai ya kutengwa kuwa eneo la wazi kwa ajili ya matumizi ya miundombinu mbalimbali ya maji safi, maji taka na njia za kupitisha maji ya mvua.
Walisema wanataka TAKUKURU ichunguze mazingira ya mabadiliko ya matumizi ya eneo hilo, nyaraka za umiliki na vibali vilivyotumika kuruhusu ujenzi huo ili kubaini kama taratibu za kisheria zilifuatwa.
Wasiwasi wa wakazi hao umeongezeka kufuatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu matarajio ya mvua za El Niño, wakieleza kuwa ujenzi huo unaweza kuathiri upitishaji wa maji ya mvua na kuongeza changamoto za mafuriko endapo njia zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maji zitazibwa.
Aidha, wakazi hao wanadai kuwa ujenzi huo haujakamilisha taratibu zote za kimazingira, ikiwemo kupata kibali kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Kwa mujibu wa maelezo yao, baada ya malalamiko kuwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya, iliundwa kamati iliyofanya uchunguzi na kubaini kuwa ujenzi huo haukufuata matakwa ya tathmini ya athari kwa mazingira.
Kamati hiyo inadaiwa kuandaa ripoti na kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ikipendekeza kusimamishwa kwa ujenzi huo hadi tathmini ya athari za kimazingira ifanyike.
Hata hivyo, viongozi hao walisema mapendekezo hayo yanadaiwa kutofikishwa kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, hali inayowafanya kuomba hatua zaidi zichukuliwe ili kupata ufafanuzi wa kisheria kuhusu ujenzi huo.
Wamesisitiza kuwa lengo lao si kuzuia maendeleo ya uwekezaji, bali kuhakikisha ujenzi unazingatia sheria, matumizi yaliyopangwa ya ardhi na usalama wa miundombinu inayohudumia wananchi.
Wakatoa wito kwa TAKUKURU, NEMC na uongozi wa Jiji la Arusha kufanya uchunguzi wa pamoja ili kubaini uhalali wa umiliki wa eneo hilo, vibali vya ujenzi na utekelezaji wa mapendekezo ya kamati iliyoundwa kuchunguza malalamiko hayo.
Wakazi hao wameeleza kuwa wanahitaji majibu ya wazi kuhusu hatma ya eneo hilo, wakisisitiza kuwa athari za kuzibwa kwa njia za maji zinaweza kuwakumba wananchi wengi endapo hatua za tahadhari hazitachukuliwa.
Ends

إرسال تعليق