Ad
Breaking🔥

MWANAMKE AUAWA KWA KUKATWA SHINGO, KUDUNGWA VISU ARUSHA

 MWANAMKE AUAWA KWA KUKATWA SHINGO, KUDUNGWA VISU ARUSHA

Na Joseph Ngilisho-ARUMERU

MWANAMKE aliyefahamika kwa jina maarufu la Mama Shio (46), mfanyabiashara wa supu katika eneo la Usariver Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ameuawa baada ya kukatwa shingo na kudungwa visu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mwanaume aliyekuwa akiishi naye, anayefahamika kwa jina la Gudi (35), anadaiwa kuhusishwa na tukio hilo, ambalo kwa mujibu wa taarifa za awali linahusishwa na wivu wa kimapenzi.

Kwa mujibu wa majirani, marehemu na mwanaume huyo walikuwa na migogoro ya mara kwa mara. Walisema usiku wa kuamkia leo, majira ya saa saba, walisikia sauti za ugomvi kutoka nyumbani kwao, lakini hawakuchukua hatua yoyote wakidhani ni mzozo wao wa kawaida.

Mwili wa Mama Shio uligunduliwa asubuhi na rafiki yake aliyekuwa amemfuata kwa ajili ya kwenda kazini baada ya kumkosa na kushindwa kumpata kupitia simu yake ya mkononi.

Rafiki huyo alielekea nyumbani kwa marehemu, lakini baada ya kugonga mlango bila kupata majibu, alizunguka upande wa nyuma wa nyumba na kuingia kupitia dirisha lililokuwa wazi.

Alipoingia ndani na kufungua pazia, alikumbana na mwili wa Mama Shio ukiwa uchi, ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali, huku chumba kikiwa kimetapakaa damu.

Baada ya kubaini tukio hilo, majirani walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambao walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi kabla ya kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Tukio hilo limeibua hofu na masikitiko miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kutokana na namna mwanamke huyo alivyopoteza maisha.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم