LUKUMAY AWALETA WABUNGE WA DUNIA (IPU) ARUMERU MAGHARIBI, WAJENGA ZAHANATI YA KISASA YA MILIONI 264 ILKIDING'A
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akipongeza uwekezaji unaofanywa na Tanzania Horticultural Association (TAHA) katika kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kipato.
Dkt Lukumay alisema hayo OKTOBA 6,2026 wakati Kamati ya Maendeleo ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ilipotembelea mradi wa mfereji wa umwagiliaji unaofadhiliwa na TAHA katika Kata ya Ilkiding’a, Jimbo la Arumeru Magharibi.
Alisema Serikali imeweka msisitizo katika kushirikisha sekta binafsi katika maendeleo ya nchi, akisema uwekezaji wa aina hiyo ni sehemu muhimu ya kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Sekta binafsi inaenda kufanya kwa asilimia 70 katika utekelezaji wa dira yetu. Kwa hiyo tunapaswa kuendelea kuishirikisha na kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kufanya kazi kubwa zaidi katika kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema mradi huo umeanza kuonyesha matokeo, akieleza kuwa wakulima wameongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa vitunguu tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
“Tumepata habari kwamba kabla TAHA haijaingia, ekari moja ya vitunguu ilikuwa ikitoa takribani magunia 10, lakini sasa wamefikia magunia 50. Hii inaonyesha maendeleo makubwa na faida ambayo wananchi wetu wanaipata,” alisema.
Alisema uwekezaji huo pia umefungua fursa kwa vijana na wananchi kupata ajira na kuongeza kipato, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.
Dkt Lukumay pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za Serikali katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi, ikiwamo kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuharakisha miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi, akilenga maendeleo ya miundombinu, kuimarisha nguvu kazi na kuboresha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi,” alisema.
Aidha, Dkt Lukumay aliwashukuru wajumbe wa IPU kwa kutenga muda kutembelea eneo hilo na kujionea namna uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji unavyobadili maisha ya wananchi.
“Tunawashukuru sana kwa kuchukua muda wenu kuja kutembelea eneo hili na kuwaona wananchi wetu. Tunathamini sana muda wenu na tunafurahi kuwa mmeweza kujionea maendeleo yanayofanyika hapa,” alisema.







Post a Comment