Ad

DC LUGANGIRA AANZA KUISUKA ARUMERU YA KIMATAIFA ,APOKEA WABUNGE WAZITO WA IPU

DC LUGANGIRA AANZA KUISUKA ARUMERU YA KIMATAIFA  ,APOKEA  WABUNGE WAZITO  WA IPU

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amepokea kundi la wabunge kutoka mataifa 16 wanaoshiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), waliotembelea miradi ya afya na kilimo katika Halmashauri ya Arusha.

Wabunge hao walitembelea Mradi wa Zahanati ya Kioga pamoja na mradi wa umwagiliaji unaowanufaisha vijana katika Kijiji cha Oloigeruno, wakijionea namna miradi hiyo inavyosaidia kuboresha huduma za afya na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.


Lugangira aliwapongeza wajumbe hao kwa kuonyesha dhamira ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, akisema ushirikiano huo unapaswa kupanuliwa hadi maeneo mengine yenye mahitaji ya huduma za afya na kilimo.

“Sisi kama Arumeru tupo tayari kuendeleza ushirikiano huu na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, yakiwamo UNICEF, WHO na WFP, pamoja na Mastercard Foundation na TAHA. Ombi langu kubwa ni miradi hii ifike maeneo mengine hapa Arusha DC na, kwa kuwa Wilaya yetu ina Halmashauri mbili, ni muhimu pia tufike Meru DC ili kuhakikisha tunachangia matokeo chanya na endelevu kwa wananchi wetu,” alisema Lugangira.

Alisema ziara hiyo imekuwa fursa kwa wajumbe hao kuona kwa vitendo namna ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo unavyoweza kuleta matokeo katika huduma za msingi, hususan afya ya mama na mtoto pamoja na kilimo cha umwagiliaji kwa vijana.

Kwa upande wake, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa, Hoyce Anderson Temu, alisema Tanzania imepata heshima kubwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU na inapaswa kutumia fursa hiyo kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kimataifa.

“Mkutano huu ni mlango wa kufungua ushirikiano na nchi mbalimbali duniani, hivyo naendelea kusisitiza usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali na wadau wengine,” alisema Temu.

Wajumbe hao walipata pia fursa ya kujionea utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Kioga, pamoja na shughuli za vijana katika mradi wa umwagiliaji na kilimo cha mbogamboga.

Mkutano wa 153 wa IPU unaendelea jijini Arusha, ukiwakutanisha wabunge na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post