IPU YAPONGEZA MRADI WA TAHA WA UMWAGILIAJI ARUMERU MAGHARIBI
.....Wajumbe wajionea namna zaidi ya wananchi 1,200 wanavyonufaika na kilimo cha umwagiliaji
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Pongezi hizo zilitolewa na mwakilishi wa IPU, Valentine Ceuteno, baada ya wajumbe wa umoja huo kutoka sehemu mbalimbali duniani kutembelea mradi huo na kujionea namna mfereji wa umwagiliaji unavyowawezesha wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani, ikiwamo vitunguu.
Ceuteno alisema ziara hiyo imewapa wajumbe fursa ya kuona kwa vitendo matokeo ya miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, akipongeza Serikali, Umoja wa Mataifa (UN), mashirika yake pamoja na sekta binafsi kwa juhudi hizo.
“Tunashukuru sana kuwa hapa. Tumekuja kama wawakilishi wa IPU kutoka Kamati ya Umoja wa Mataifa na Kamati ya Afya, na tunawapongeza viongozi na mamlaka za eneo hili kwa kazi mnayoifanya,” alisema.
Alisema ushirikiano wa taasisi za UN, zikiwamo WFP na UNICEF, pamoja na TAHA kama mdau wa sekta binafsi, una mchango katika kuboresha maisha ya jamii.
“Tunajisikia kuhamasika, tuna matumaini na tunafurahi. Jambo muhimu zaidi ni kwamba kazi yote tunayofanya inalenga maslahi bora ya watoto wetu na ustawi wa kizazi cha watoto,” alisema Ceuteno.
Wananchi 1,200 wanufaika
Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, alisema zaidi ya wananchi 1,200 wananufaika na mradi huo wa mfereji wa umwagiliaji, ambao umefungua fursa mpya za uzalishaji kwa wakulima katika Jimbo la Arumeru Magharibi.
Alisema upatikanaji wa maji ya uhakika umewawezesha wakulima kuongeza maeneo ya kilimo, kulima kwa misimu inayofuatana na kuongeza kipato, huku ukiwapa vijana fursa za ajira katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na kilimo.
“Jukumu letu ni kusaidia maendeleo na mabadiliko ya sekta ya kilimo cha bustani. Tunafanya kazi kwa karibu sana na Serikali kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki kwa wakulima na sekta binafsi,” alisema Dkt. Mkindi.
Alisema TAHA pia imekuwa ikifanya kazi ya kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa kuongeza uzalishaji lazima kuambatane na uhakika wa masoko.
“Katika kilimo huwezi kuzungumzia mnyororo wa thamani wenye ushindani bila masoko na biashara. Sisi tunafungua masoko, tunawezesha biashara na tunabaini fursa za uwekezaji,” alisema.
Dkt. Mkindi alisema TAHA imekuwa ikifanya tafiti za masoko na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa, ikiwamo India, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la dunia.
‘Maji yametubadilishia maisha’
Mkulima Godlizen Michael Mollel, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, alisema upatikanaji wa maji ya uhakika umeondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakulima na kuwawezesha kutumia maeneo yao kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Kwa kweli mradi huu tumenufaika sana. Awali tulikuwa na eneo kubwa la kulima, lakini tulikuwa tunakosa maji ya uhakika. Sasa tunapata maji ya kumwagilia, matumizi ya nyumbani na hata kwa ajili ya mifugo,” alisema Mollel.
Alisema wakulima sasa wanaweza kulima mazao mbalimbali kwa misimu inayofuatana, yakiwamo mahindi na kabichi, jambo alilosema limeongeza uzalishaji na kipato cha kaya.
Ziara ya wajumbe wa IPU imeifanya Arumeru Magharibi kuwa miongoni mwa maeneo maarufu ambayo wajumbe hao wamepata fursa ya kujionea kwa vitendo namna uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji unavyoweza kuchochea uzalishaji, ajira na kipato kwa wananchi.
Ends












إرسال تعليق