Ad
Breaking🔥

EALA YATAKA NCHI ZA EAC KUDHIBITI VIUATILIFU HATARISHI

 EALA YATAKA NCHI ZA EAC KUDHIBITI VIUATILIFU HATARISHI

...Lataka Baraza la Mawaziri kuharakisha mkakati wa miaka 10, kuimarisha usimamizi na kupambana na biashara ya viuatilifu bandia

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

BUNGE la Afrika Mashariki (EALA) limetaka Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama kuharakisha utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti viuatilifu vyenye hatari kubwa, huku likisisitiza umuhimu wa kuimarisha sheria, usimamizi na matumizi ya njia mbadala zilizo salama kwa afya ya binadamu na mazingira.

Katika azimio lililowasilishwa na Mbunge wa EALA, Caroline Rwivanga Kayonga, Bunge hilo limetaka utekelezaji wa Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Usimamizi wa Viuatilifu Vyenye Hatari Kubwa wa mwaka 2026–2036 kupewa kipaumbele katika sera na mipango ya kitaifa na kikanda.



Azimio hilo pia limelitaka Baraza la Mawaziri na nchi wanachama kuhakikisha zinatenga rasilimali za kutosha za kifedha na kitaalamu ili kuwezesha utekelezaji wa mkakati huo, unaolenga kutambua, kutathmini na kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya viuatilifu hatarishi.

Hoja hiyo imewasilishwa kwa mujibu wa masharti mbalimbali ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanuni za Kudumu za Bunge hilo, ikisisitiza wajibu wa nchi wanachama kushirikiana katika kilimo, usalama wa chakula, utunzaji wa mazingira na ulinzi wa afya ya umma.

Katika azimio hilo, EALA limeeleza kuwa pamoja na nchi wanachama kuwa na mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi inayosimamia usajili, uingizaji, usambazaji na matumizi ya viuatilifu, bado kuna tofauti katika udhibiti na utekelezaji wa sheria kati ya nchi hizo.

Bunge hilo limeonya kuwa mapungufu ya udhibiti, uwezo mdogo wa maabara, uelewa usiotosheleza wa hatari za viuatilifu na biashara haramu ya viuatilifu bandia ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuhatarisha afya ya binadamu na mazingira.

Aidha, kuendelea kusambaa kwa viuatilifu vilivyopigwa marufuku au vyenye hatari kubwa kunaweza kuathiri bioanuwai, ubora wa maji na udongo, mifumo ya chakula, uzalishaji endelevu wa kilimo na biashara ya kikanda.

Kutokana na hali hiyo, azimio linataka nchi wanachama kuoanisha hatua zao za udhibiti na viwango vilivyokubaliwa na EAC, kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa, kufanya tathmini za hatari kwa ushirikiano na kuratibu utekelezaji wa sheria katika kukabiliana na biashara haramu ya viuatilifu bandia.

EALA pia limehimiza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya nchi wanachama ili kupunguza mianya inayoweza kutumiwa na wafanyabiashara kuingiza au kusambaza bidhaa hizo kinyume cha sheria.

Katika eneo la uzalishaji wa kilimo, azimio hilo linataka nchi wanachama kuweka mfumo wa mpito wa hatua kwa hatua kuelekea matumizi ya njia salama na endelevu za kudhibiti visumbufu vya mimea.

Njia zinazopendekezwa ni pamoja na udhibiti jumuishi wa visumbufu vya mimea, matumizi ya viuatilifu vinavyotokana na viumbe hai na mbinu za kilimo ikolojia, sambamba na kuimarisha utafiti, huduma za ugani na msaada kwa wakulima na wadau wengine wa mnyororo wa thamani.

Azimio hilo linasisitiza kuwa mabadiliko hayo yanapaswa kuzingatia mazingira ya wakulima na kuwezeshwa kwa rasilimali za kutosha, ili kuimarisha uzalishaji wa kilimo bila kuongeza hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Aidha, Bunge limetaka kuanzishwa na kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji, uwajibikaji, ushiriki wa wadau na utoaji wa taarifa za mara kwa mara kwa Baraza la Kisekta husika, ili kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huo unafuatiliwa kwa ufanisi katika ngazi za kitaifa na kikanda.

Mkakati huo wa miaka 10, uliopitishwa Julai 10, 2026, umeelezwa katika azimio hilo kuwa mfumo muhimu wa pamoja wa EAC wa kupunguza hatari zinazotokana na viuatilifu vyenye madhara makubwa.

Hoja hiyo, iliyowasilishwa na Kayonga, iliungwa mkono na Mbunge wa EALA George Stephen Odongo.

Azimio hilo linatokana na wajibu wa nchi wanachama kushirikiana katika kuimarisha usalama wa chakula, kulinda mazingira na afya ya umma, huku likitambua mchango wa vyama vya wakulima, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na wataalamu katika kupunguza hatari zinazotokana na viuatilifu.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post