Ad
Breaking🔥

EAC YAPOKEA MSAADA WA DOLA 180,000 KUTOKA CHINA ,YAITAKA KUPANUA MSAADA ZAIDI KATIKA MIUNDOMBINU

 EAC YATAKA CHINA KUPANUA MSAADA WAKE KATIKA MIUNDOMBINU

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeiomba Serikali ya China kupanua ushirikiano wake na jumuiya hiyo kutoka katika kujenga uwezo wa taasisi hadi kusaidia miradi ya miundombinu, biashara, nishati safi, teknolojia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ombi hilo limetolewa OKTOBA 5,2026 na Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi, wakati wakitiliana saini mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya EAC,kuhusu ushirikiano kati ya jumuiya hiyo na China, ikiwamo msaada wa dola 180,000 za Marekani unaotolewa na Serikali ya China kila mwaka kwa ajili ya kusaidia shughuli za EAC.

Balozi Mbundi alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia shughuli mbalimbali za jumuiya, zikiwemo ufuatiliaji wa uchaguzi, maonesho ya biashara kwa wajasiriamali wadogo, kujenga uwezo wa watumishi na kuimarisha mawasiliano kuhusu ajenda ya ujumuishaji wa kikanda.

“Tunashukuru na kuthamini mchango huu. Msaada wa China umefika hadi ngazi ya chini kupitia kusaidia maonesho ya Jua Kali, hivyo unaonekana moja kwa moja kwa wananchi,” alisema.

Alisema EAC sasa inataka ushirikiano huo uelekezwe zaidi katika miradi inayoweza kuharakisha maendeleo na kuunganisha nchi wanachama, ikiwamo miundombinu ya biashara na usafirishaji, viwanda na kuongeza thamani, nishati safi, biashara ya kidijitali, usalama wa chakula na ujenzi wa uwezo wa taasisi.

Balozi Mbundi alisema EAC pia inaomba China kuendelea kusaidia upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA pamoja na kupanua mafunzo ya kitaalamu kwa watumishi wa jumuiya hiyo.



Alisema ushirikiano kati ya EAC na China haujajikita kwenye fedha pekee, bali pia umehusisha mafunzo, kubadilishana uzoefu na misaada ya vifaa.

Alitoa mfano wa magari manane yaliyotolewa na Serikali ya China mwaka 2023, yenye thamani ya takribani dola 400,000 za Marekani, ambayo yamekuwa yakitumika kusaidia shughuli za EAC na baadhi ya taasisi nyingine za kikanda.

“Magari haya hayasaidii EAC pekee. Moja limepelekwa Tume ya Bonde la Ziwa Victoria na mengine yanatumika katika shughuli mbalimbali. Hata tunapokuwa na mikutano mikubwa hapa, waandaaji huja kwetu na kuyaomba kwa matumizi yao,” alisema.

Alisema mwaka huu maofisa wa EAC walishiriki semina mjini Beijing kuhusu uchumi wa kijani na uhifadhi wa mazingira kupitia Mpango wa Maendeleo ya Dunia (GDI), hatua aliyosema imeongeza uelewa na kubadilishana uzoefu kati ya pande hizo.

Kwa mujibu wa Balozi Mbundi, EAC inapendekeza kuanzishwa kwa mazungumzo maalumu kati yake na China yatakayolenga kubaini miradi ya kikanda yenye kipaumbele na kuweka mazingira ya ushirikiano katika fedha, teknolojia, uhamishaji wa maarifa na ushiriki wa sekta binafsi.

“Tunakaribisha ushirikiano unaounganisha fedha, teknolojia, uhamishaji wa maarifa, ujenzi wa uwezo na ushiriki wa sekta binafsi,” alisema.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya EAC, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema Serikali yake itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo katika kuimarisha ujumuishaji wa kikanda na maendeleo ya nchi wanachama.

Alisema China imetoa dola 180,000 za Marekani kwa EAC kwa ajili ya kujenga uwezo na kusaidia bajeti na shughuli za jumuiya hiyo.

“China inafurahi kutoa dola 180,000 za Marekani kwa EAC kwa ajili ya kujenga uwezo na bajeti,” alisema.

Balozi Chen alisema China inatambua hatua ambazo EAC imepiga katika mchakato wa ujumuishaji wa kikanda na iko tayari kuendelea kushirikiana na jumuiya hiyo kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi wanachama.

Alisema ziara yake inamkumbusha ya mwaka 2023 alipofika katika Makao Makuu ya EAC kukabidhi magari yaliyotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya kusaidia shughuli za jumuiya.

“China inathamini maendeleo hayo na tuko tayari kushirikiana na EAC kwa ajili ya ustawi na maendeleo zaidi ya jumuiya hii pamoja na nchi zote wanachama,” alisema.

Balozi Mbundi alisema EAC itaendelea kuhakikisha misaada inayotolewa na China inatumika kwa uwazi na uwajibikaji, huku ikilenga kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.

Alisema EAC ni jumuiya inayomweka mwananchi katikati na inayochochewa na soko, hivyo ushirikiano na China unapaswa kuelekezwa kwenye miradi yenye manufaa yanayoonekana katika nchi wanachama.

“Tunataka kuona fedha hii ikitafsiri malengo yaliyopo kwenye mpango wetu wa kimkakati na kuhakikisha inafika hadi ngazi ya wananchi, ambao ndio msingi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.

Aidha, Balozi Mbundi alisema EAC inaunga mkono sera ya China ya “China Moja”, akieleza kuwa jumuiya hiyo inaweza kujifunza kutoka China katika safari yake ya kuelekea kuwa shirikisho la kisiasa.

“EAC inalenga kuwa shirikisho la kisiasa, ambapo tutakuwa na kituo kimoja cha kisiasa. Kwa mantiki hiyo, tunaunga mkono sera ya China Moja kwa sababu tunaona kuna mambo yanayofanana na tuna mengi ya kujifunza kutoka China,” alisema.

Alisema vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Dunia (GDI) vinaendana na Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC unaolenga kuharakisha maendeleo ya nchi wanachama.

Balozi Mbundi aliishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuunga mkono ajenda ya ujumuishaji wa Afrika Mashariki, akisema EAC ipo tayari kuimarisha zaidi ushirikiano huo.

Ends..


Post a Comment

أحدث أقدم