Ad
Breaking🔥

MAHAKAMA YAAMURU IGP, KULIPA SH646 MILIONI

MAHAKAMA YAAMURU IGP, TANESCO KULIPA SH646 MILIONI

Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuilipa kampuni ya Future Century Limited Sh646 milioni, baada ya kubainika kuwa sehemu ya vifaa vya umeme vilivyokamatwa na polisi mwaka 2006 haikurejeshwa.

Hukumu hiyo iliyotolewa Septemba 24, 2026 na Jaji Hamidu Mwanga, imeamuru walalamikiwa hao kulipa Sh596 milioni, ikiwa ni thamani ya vifaa vilivyodaiwa kupotea, pamoja na Sh50 milioni kama fidia ya jumla.

Aidha, Mahakama imeamuru kiasi hicho kilipwe kikiwa na riba ya asilimia saba kwa mwaka, kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo yote yatakapokamilika, sambamba na gharama za shauri.

Mgogoro huo ulianza Julai 2006 baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kuwa kampuni hiyo ilikuwa inamiliki vifaa na zana za umeme vilivyodhaniwa kuibwa kutoka Tanesco.

Baada ya taarifa hiyo, polisi walimkamata mmoja wa wakurugenzi wa Future Century Limited na kufanya upekuzi katika eneo la biashara la kampuni hiyo, Mikocheni, Dar es Salaam, ambapo walikamata vifaa, mitambo na zana 57 kwa ajili ya uchunguzi.

Kwa mujibu wa madai ya kampuni hiyo, baada ya uchunguzi kukamilika, polisi hawakupata ushahidi wa kutosha wa kuanzisha mashtaka ya jinai, hivyo jalada lilifungwa.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa Tanesco kwa ajili ya kuhifadhiwa, lakini Januari 18, 2012, wakati wa makabidhiano, kampuni hiyo ilidai kuwa ilirejeshewa vifaa 13 pekee kati ya 57 vilivyokuwa vimekamatwa.

Hali hiyo ilisababisha kampuni hiyo kudai fidia ya thamani ya vifaa vilivyodaiwa kutorejeshwa, madai ambayo yalipingwa na IGP pamoja na Tanesco.

Katika utetezi wao, walidai kuwa vifaa vyote vilivyokamatwa vilirejeshwa baada ya uchunguzi kukamilika na kwamba hawakuwajibika kwa vifaa vilivyodaiwa kupotea.

Pia walipinga madai ya fidia na riba, wakisisitiza kuwa hayakuwa na msingi na kwamba hakukuwa na makubaliano wala ahadi ya kurejesha vifaa kwa namna iliyodaiwa na Future Century Limited.

Hata hivyo, katika hukumu yake, Jaji Mwanga alisema ushahidi uliowasilishwa Mahakamani ulithibitisha kuwa polisi walikamata vifaa 57 na kwamba vifaa hivyo viliwekwa chini ya uangalizi wa Tanesco.

Mahakama ilibaini pia kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha unaoonyesha namna vifaa vyote 57 vilivyokamatwa vilivyolinganishwa na vifaa 13 vilivyokabidhiwa kwa kampuni hiyo mwaka 2012.

Kwa msingi huo, Mahakama ilifikia uamuzi wa kuwataka IGP na Tanesco kuwajibika kwa malipo hayo, pamoja na fidia na riba kama ilivyoainishwa katika hukumu.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم