MFANYABIASHARA WICKNELL CHIVAYO, MKEWE WAFARIKI AJALI YA HELIKOPTA ZIMBABWE
By Arushadigital-HARARE, Zimbabwe —
Mfanyabiashara maarufu nchini Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mke wake, Lucy “Lulu” Muteke, wamefariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea eneo la Marondera Rural, mashariki mwa mji mkuu Harare.
Kifo cha wanandoa hao kimethibitishwa na msemaji wa familia, Herbert Chivayo, huku mamlaka za Zimbabwe zikisema watu wote waliokuwa ndani ya helikopta hiyo hawakunusurika.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano, Septemba 30, 2026, majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Zimbabwe, wakati helikopta hiyo ilipoanguka katika eneo la Marondera Rural. Polisi nchini humo walithibitisha kuwa kulikuwa na watu sita ndani ya ndege hiyo wakati wa ajali.
Kwa mujibu wa taarifa za familia na vyombo vya habari nchini Zimbabwe, Chivayo na mke wake walikuwa miongoni mwa watu sita waliofariki katika ajali hiyo.
Jeshi la Polisi la Zimbabwe (ZRP) limeendelea na taratibu za utambuzi wa miili, huku likisema taarifa zaidi kuhusu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo zitatolewa baada ya uchunguzi wa eneo la tukio kukamilika.
Msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana, amesema hakukuwa na manusura katika ajali hiyo, huku taarifa zikieleza kuwa miili ya baadhi ya wahanga iliharibiwa vibaya na moto uliotokea baada ya helikopta kuanguka.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijatangazwa rasmi, huku mamlaka zikiendelea na uchunguzi wa kubaini mazingira yaliyosababisha helikopta hiyo kuanguka.
Chivayo, aliyekuwa na umri wa miaka 43, alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara waliotambulika sana nchini Zimbabwe, akijulikana kwa shughuli zake za biashara pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii na michango kwa taasisi na watu mbalimbali.
Tukio hilo limezua simanzi nchini Zimbabwe huku familia, mamlaka na jamii zikisubiri kukamilika kwa taratibu za utambuzi wa wahanga na uchunguzi wa ajali hiyo.
Ends





Post a Comment