THRDC, MAIPAC WAWANOA WAANDISHI WA MAZINGIRA KANDA YA KATI
Na Mwandishi Wetu | ARUSHA DIGITAL, DODOMA
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), umewataka waandishi wa habari nchini kuongeza nguvu katika uandishi wa habari za mazingira, hasa kwa kufanya uchunguzi unaobaini chanzo cha changamoto na kueleza suluhisho zake.Wito huo umetolewa jijini Dodoma jana, Septemba 22, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari za mazingira yanayolenga kuwajengea uwezo wa kutumia taaluma yao kuongeza uwajibikaji, uelewa wa umma na ulinzi wa haki za binadamu katika masuala ya mazingira.
Mafunzo hayo yanaendeshwa kupitia mradi wa “Kuwawezesha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania kuwa na Athari Endelevu,” unaodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), na unawaleta pamoja waandishi kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Morogoro na Iringa.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa, alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za mazingira ambazo, licha ya kuathiri maisha ya wananchi, hazipewi uzito unaostahili katika uandishi wa habari.
Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni uchafuzi wa mazingira mijini, uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji pamoja na uwekezaji usiozingatia kikamilifu athari za kimazingira.
Wakili Ole Ngurumwa alisema hali ya usafi katika baadhi ya maeneo ya mijini ni miongoni mwa masuala yanayohitaji waandishi kuyafuatilia kwa kina na kuwafikisha wahusika mbele ya jamii.
“Rais Samia alisema Dar es Salaam ni chafu, mimi nasema inanuka, kwani uchafu umesambaa kila kona,” alisema.
Alisema waandishi hawapaswi kuishia kuripoti uwepo wa tatizo, bali wanapaswa kuchunguza chanzo chake, kubaini wahusika, kufuatilia hatua zinazochukuliwa na kueleza namna changamoto hizo zinavyoweza kutatuliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, alisema dunia ipo katika kipindi kigumu kutokana na kuongezeka kwa changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, hivyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kusaidia jamii kuelewa na kukabiliana na hali hiyo.
Juma alisema Tanzania imekuwa ikikabiliwa na athari mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi, ikiwamo tishio la mvua kubwa, ukame unaoathiri maisha ya wananchi na mifugo, pamoja na changamoto nyingine zinazohusiana na mazingira.
Alisema licha ya changamoto hizo, bado kuna uhitaji wa kuongezeka kwa habari za kina na za uchunguzi zinazoweza kusaidia jamii kuelewa ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua.
“Kupitia mradi huu, nendeni mkaandike habari za uchunguzi, mubainishe changamoto za mazingira, lakini pia mueleze suluhisho na ubunifu ili kusaidia jamii,” alisema Juma.
Alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari katika uzalishaji na upatikanaji wa chakula, yamesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali na kuchangia kuibuka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Aidha, alisema wanahabari wanapaswa kutumia nafasi waliyonayo kuibua masuala hayo kwa ushahidi na kwa kuzingatia weledi ili kusaidia watunga sera, Serikali na jamii kupata taarifa zitakazowezesha kuchukua hatua.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Utetezi wa THRDC, Wakili Paul Kisabo, aliwafundisha waandishi sheria mbalimbali za ndani na za kimataifa zinazohusu ulinzi na uhifadhi wa mazingira.
Wakili Kisabo aliwataka waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa ujasiri, kuchunguza changamoto za mazingira na kuziwasilisha kwa umma bila hofu, huku wakizingatia sheria, maadili ya uandishi wa habari na ushahidi.
Alisema waandishi wana jukumu la kutumia taaluma yao kulinda maslahi ya jamii na kwamba watakapokabiliwa na changamoto kutokana na kazi zao za uandishi wa habari za mazingira, taasisi husika za utetezi ziko tayari kuwasaidia.
Mafunzo hayo yanashirikisha jumla ya waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Kati.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha waandishi wa habari kuwa na ujuzi zaidi katika uchunguzi, uandishi na ufuatiliaji wa masuala ya mazingira ili habari wanazozalisha zisibaki katika kutoa taarifa pekee, bali ziwe sehemu ya mijadala na hatua za kutafuta suluhisho la changamoto zinazozikabili jamii.
Ends







إرسال تعليق