Ad
Breaking🔥

TANROADS YAFUFUA MATUMAINI BARABARA YA KIA–ARUSHA

TANROADS YAFUFUA MATUMAINI BARABARA YA KIA–ARUSHA

.....Sh4 bilioni zatengwa kukabili mafuriko, ukarabati mkubwa waendelea

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) umesema umejipanga kuhakikisha barabara ya Kia–Arusha, inayotumiwa na maelfu ya wananchi, watalii na wafanyabiashara katika ukanda wa Kaskazini, inarejea katika hali yake nzuri baada ya kuanza kwa matengenezo makubwa katika maeneo mbalimbali.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, alisema hayo  wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya matengenezo ya barabara hiyo iliyofanywa na uongozi wa Wizara ya Ujenzi ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Dkt Charles Msonde.

Alisema matengenezo hayo yanalenga kurejesha ubora wa barabara hiyo baada ya wananchi kwa muda mrefu kulalamikia hali yake, huku Serikali ikitenga fedha kuhakikisha changamoto zilizopo zinaondolewa.

Alisema kazi hiyo inatekelezwa na wakandarasi wazawa, akiwamo Roktronic na Kings Builders, ambao wamepewa jukumu la kufanya matengenezo makubwa na kuhakikisha barabara hiyo inarejea katika kiwango kinachokidhi mahitaji ya watumiaji.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha hali ya barabara hii inarudi kama ilivyokuwa awali na inaendelea kutoa huduma ambayo wananchi wanaitarajia,” alisema Besta.

Alisema barabara hiyo ilijengwa mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa ufadhili wa Serikali ya Norway, huku wataalamu kutoka Norway kupitia kampuni ya Norconsult wakihusika katika usimamizi wa kitaalamu na kampuni ya Italia ikifanya ujenzi.

Alisema baada ya kutumika kwa miaka mingi, barabara hiyo imehitaji matengenezo makubwa na Serikali imeamua kutumia wakandarasi wa ndani katika kazi hiyo.

KIUNGO CHA NCHI ZA KASKAZINI

Besta alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kiuchumi kutokana na kuunganisha maeneo ya kitalii, biashara na usafirishaji katika ukanda wa Kaskazini.

Alisema pia ni kiungo muhimu kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Alisema ubora wa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa, hasa kutokana na nafasi ya sekta ya utalii katika kuingiza mapato na kuajiri wananchi.

“Utalii ni miongoni mwa sekta zinazoliingizia Taifa mapato makubwa. Kwa hiyo ubora wa miundombinu ni muhimu katika kuwavutia watalii na kurahisisha usafirishaji wa mizigo,” alisema.

Sh4 BILIONI KUKABILI MAFURIKO

Katika hatua nyingine, TANROADS imesema imetumia takribani Sh4 bilioni katika kuboresha miundombinu ya kupitisha maji katika maeneo yaliyokuwa yakikabiliwa na mafuriko wakati wa mvua kubwa.

Besta alisema fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa makalvati makubwa kupitia mpango unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, hatua ambayo inalenga kupunguza uwezekano wa maji kukwamisha matumizi ya barabara.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya maeneo ya barabara hiyo kuathiriwa na maji wakati wa mvua kubwa, hali iliyowahi kusababisha magari kushindwa kupita.

“Tumefanya maboresho katika maeneo yote yaliyokuwa yanaathiriwa na maji na tumejenga makalvati makubwa ili kuruhusu maji kupita kwa ufanisi,” alisema.

Alisema TANROADS pia inaendelea kujenga mifereji mikubwa katika maeneo mengine ili maji yaweze kupita kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine bila kuingia kwenye barabara na kusababisha mafuriko.

Besta alisema TANROADS imejiandaa pia kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua zinazotarajiwa katika kipindi hiki hadi Desemba.

Alisema timu maalumu za dharura zimeandaliwa ili kuchukua hatua haraka endapo kutatokea uharibifu wa barabara au changamoto nyingine zinazoweza kuathiri usafiri.

Alisema Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Masawe, pamoja na timu yake, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali kubaini sehemu zinazoweza kuwa hatarishi wakati wa mvua.

Alisema maandalizi hayo hayajaishia upande wa Arusha, bali yamehusisha pia maeneo ya barabara kutoka Kia kuelekea Kilimanjaro ambayo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto za mafuriko.

“Tumeshajipanga kwa ajili ya mvua. Kuna timu za dharura ambazo zipo tayari na kazi zinaendelea kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,” alisema.

Alisema TANROADS itaendelea na matengenezo hayo hadi barabara hiyo irejee katika hali inayokidhi matarajio ya wananchi na watumiaji wengine, wakiwamo watalii na wafanyabiashara wanaotegemea barabara hiyo kila siku.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم