SERIKALI KUANZISHA SHERIA YA UKAGUZI WA NDANI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeanza mchakato wa kuanzisha sheria mahsusi ya ukaguzi wa ndani, hatua inayolenga kuimarisha uhuru, mamlaka na uwajibikaji wa wakaguzi pamoja na kamati za ukaguzi nchini.Hatua hiyo imekuja huku Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiwataka wakaguzi wa ndani kubadili mtazamo wa utendaji kwa kwenda zaidi ya kuhakiki mifumo na uzingatiaji wa sheria, badala yake wawe washauri wa kimkakati wanaotoa maarifa, ushauri na ubunifu wa kuongeza tija katika taasisi.
Dkt. Nchemba alisema wakaguzi wanapaswa kuwa na weledi, uadilifu na ubunifu, huku wakipewa uwezo na mamlaka stahiki ya kupata taarifa wanazohitaji ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.Alisema wakaguzi pia wanapaswa kushirikiana na Kamati za Bunge na wadau wengine muhimu ili kuhakikisha taarifa za ukaguzi zinatumika kuboresha usimamizi wa taasisi na matumizi ya rasilimali za umma.
Hotuba ya Waziri Mkuu iliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya.
Dkt. Nchemba alisema mabadiliko ya mazingira ya utendaji, ongezeko la matarajio ya wananchi na wadau, vitisho vya usalama wa mtandao pamoja na mabadiliko ya sheria na kanuni, yanahitaji taaluma ya ukaguzi wa ndani kubadilika na kuwa mshauri wa kimkakati kwa taasisi.
Alisema kaulimbiu ya mkutano huo, “Beyond Assurance: Driving Insight, Innovation and Trust,” inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo kwa kuwafanya wakaguzi wasibaki katika kubaini na kuripoti mapungufu, bali wasaidie taasisi kutambua vihatarishi, fursa za maboresho na namna ya kuongeza thamani.
“Mkaguzi wa ndani anapaswa kuwa mtaalamu anayeisaidia taasisi kutambua hatari, kutambua fursa za maboresho, kuimarisha udhibiti, kuboresha utendaji na kuongeza thamani,” alisema Dkt. Nchemba.
Alisema uimara wa taasisi ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa kwa kuwa udhaifu katika mifumo ya utawala na udhibiti unaweza kusababisha upotevu wa rasilimali, matumizi yasiyo na tija, udanganyifu, rushwa na kutofikiwa kwa malengo yaliyowekwa.
SHERIA YA UKAGUZI
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, alisema Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha sheria mahsusi itakayoweka msingi wa kisheria wa kuimarisha uhuru, mamlaka na uwajibikaji wa wakaguzi wa ndani na kamati za ukaguzi.
Luswetula alisema sheria hiyo itaweka wazi majukumu, mamlaka, mipaka ya utendaji na mahusiano kati ya wakaguzi wa ndani, menejimenti na kamati za ukaguzi.
“Ukaguzi wa ndani hauhitaji kuwa na wakaguzi wenye weledi na uwezo pekee, bali pia unahitaji kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kisheria unaolinda uhuru, mamlaka na uwajibikaji wa wakaguzi wa ndani pamoja na kamati za ukaguzi,” alisema.
Alisema Serikali pia inaendelea kuhuisha muundo wa kiutumishi wa kada hiyo ili kutoa nafasi kwa wataalamu wa taaluma mbalimbali, wakiwamo wahandisi na madaktari, kushiriki katika ukaguzi kulingana na vihatarishi na mahitaji ya sekta husika.
Luswetula alisema Serikali imekamilisha mifumo ya kidijitali ya ukaguzi wa ndani na usimamizi wa vihatarishi, GIAMIS na GERMIS, ambayo itasaidia kuongeza ufanisi wa ukaguzi na kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati kwa ajili ya maamuzi.
Hata hivyo, alisema kada hiyo bado inakabiliwa na changamoto za upungufu wa wataalamu na rasilimali, uhuru wa ukaguzi na kamati za ukaguzi, mabadiliko ya teknolojia pamoja na utekelezaji usioridhisha wa mapendekezo ya wakaguzi.
WATAKA UHURU
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA Tanzania), Jonathan Ngoma, alisema kuna haja ya kuimarisha uhuru wa wakaguzi ili waweze kutoa taarifa za kitaalamu bila kuingiliwa na kuhakikisha mapendekezo yao yanafanyiwa kazi.Ngoma alisema mabadiliko ya teknolojia yamepanua majukumu ya wakaguzi, ambao kwa sasa hawashughulikii fedha pekee, bali pia teknolojia, usalama wa mitandao, vihatarishi na mifumo ya udhibiti wa ndani.
Alisema baadhi ya taasisi bado zina mtazamo wa kumchukulia mkaguzi wa ndani kama mtu anayehesabu fedha, wakati taaluma hiyo ina nafasi kubwa katika utawala bora, usimamizi wa vihatarishi na maamuzi ya kimkakati.
Naye Mwenyekiti wa Mkutano wa IIA Tanzania, Dkt. Benedicto Baragomwa, alisema taasisi za Serikali na sekta binafsi zinapaswa kutumia ukaguzi wa ndani kuongeza tija, ubunifu na ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Alisema mkutano huo unatoa nafasi kwa viongozi na wataalamu kutoka sekta mbalimbali kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya taasisi ili iweze kutoa matokeo yanayotarajiwa.
Dkt. Nchemba aliwapongeza wataalamu wa ukaguzi wa ndani kwa mchango wao katika usimamizi wa fedha za umma, uwajibikaji, uadilifu na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, akisema Serikali inatambua umuhimu wa taaluma hiyo katika kujenga taasisi imara.
“Wakaguzi wa ndani wamekuwa askari wazuri wa usimamizi wa rasilimali za taifa kwa uadilifu. Hongereni sana askari wetu wa usimamizi,” alisema Dkt. Nchemba.
Ends








إرسال تعليق