MAKALLA ATAMBULISHA KONGAMANO LA TANO LA UFUATILIAJI NA TATHMINI
Na Arusha Digital | ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, ametangaza kufanyika kwa Kongamano la Tano la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini, litakalowakutanisha takribani washiriki 1,500 katika Hoteli ya Kitalii ya Ngurdoto, nje kidogo ya Jiji la Arusha, kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2026.
Makalla amesema kongamano hilo ni jukwaa la kitaifa linalolenga kuimarisha matumizi ya takwimu na ushahidi katika kufanya maamuzi, kupanga na kutekeleza mipango ya Serikali, ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija na malengo ya maendeleo yanafikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Arusha wakati akilitambulisha kongamano hilo, Makalla amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.Amesema kongamano hilo la siku tano litawakutanisha viongozi na watendaji wa Serikali, wataalamu, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, ubunifu na mbinu bora za ufuatiliaji, tathmini na matumizi ya takwimu.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Kutoka Ushahidi hadi Vitendo”, inayolenga kuhamasisha matumizi ya ushahidi unaotokana na takwimu katika kuchukua hatua na kuboresha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Makalla, moja ya malengo makubwa ya kongamano hilo ni kuhakikisha takwimu zinazokusanywa na kutumiwa na Serikali zinakuwa na tija katika kufanya maamuzi na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
UKUSANYAJI NA MATUMIZI YA TAKWIMU
Makalla amesema mada mbalimbali zitajadiliwa wakati wa kongamano hilo, ikiwemo namna bora ya kukusanya takwimu, mbinu za matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi na kufanya tathmini ya mipango iliyotekelezwa hapo nyuma.
Amesema tathmini ya mipango iliyopita ni muhimu kwa Serikali kujifunza yaliyofanyika, kubaini mafanikio na changamoto na kutumia uzoefu huo kuboresha mipango na utekelezaji wa siku zijazo.
“Tunataka kuhakikisha takwimu zinazotumika zina tija katika Serikali na zinasaidia kufikia malengo ya Dira ya 2050,” amesema Makalla.
Amesema ufuatiliaji na tathmini si zoezi la kitaalamu pekee, bali ni msingi wa kuhakikisha mipango ya Serikali inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta matokeo yanayoweza kuonekana na kupimwa.
WASHIRIKI 1,500
Makalla amesema takribani washiriki 1,500 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo, ambalo litakuwa fursa ya wadau kutoka sekta mbalimbali kukutana na kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini nchini.
Amesema jukwaa hilo pia litatoa nafasi ya kupata mrejesho kuhusu utekelezaji wa mipango ya Serikali na namna wananchi wanavyonufaika na huduma zinazotolewa.
Ameeleza kuwa ushahidi wa mafanikio ya Serikali haupaswi kubaki katika takwimu na taarifa za kiutendaji pekee, bali unapaswa kuonekana katika maisha ya wananchi kupitia huduma bora za afya, elimu, maji na huduma nyingine za kijamii.
“KUTOKA USHAHIDI HADI VITENDO”
Makalla amesema kaulimbiu ya kongamano hilo inalenga kuifanya Serikali isiishie katika kukusanya takwimu na kufanya mipango, bali itumie taarifa hizo kuchukua hatua na kufanya marekebisho pale inapobainika kuwa utekelezaji hauleti matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini unawezesha Serikali kufuatilia maendeleo, kupima matokeo na kufanya marekebisho sahihi kwa wakati.
“Utapata mrejesho ambao ni mzuri na ule ambao ni hasi, na hiyo inakuwa ni kazi ya Serikali kwenda kuendelea kuyafanyia kazi,” amesema.
Amesema kongamano hilo, pamoja na kuwa linafanyika Arusha, lina umuhimu kwa Taifa zima kwa kuwa mijadala na uzoefu utakaopatikana utalenga kuboresha namna Serikali inavyopanga, kutekeleza na kupima matokeo ya mipango yake ya maendeleo.
Makalla amewaalika washiriki wote kufika Arusha, akisema mkoa huo una sifa ya ukarimu, amani na utulivu, huku akiwataka waandishi wa habari kufuatilia na kuhabarisha umma kuhusu mijadala na matokeo ya kongamano hilo.
Ends


إرسال تعليق