Breaking🔥

SAMIA KUZINDUA RAMANI YA KUOKOA MAMA NA WATOTO AFRIKA,

SAMIA KUZINDUA RAMANI YA KUOKOA MAMA NA WATOTO AFRIKA

.....Ajenda ya “Sifuri Tatu” yaweka mkakati wa kumaliza vifo vinavyoweza kuzuilika

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, anatarajiwa kuzindua Ramani ya Utekelezaji ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto na Vijana 2026–2030, Septemba 9, 2026, jijini Arusha.

Uzinduzi huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Huduma za Afya ya Msingi, kwa kushirikiana na Africa CDC, ukiweka msukumo mpya wa utekelezaji wa ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.

Ramani hiyo inalenga kuunganisha dhamira za kisiasa za viongozi wa Afrika na utekelezaji wa vitendo katika nchi wanachama, kwa kuimarisha huduma za afya ya msingi, mifumo ya rufaa za dharura, huduma salama za uzazi, chanjo na uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya.

“SIFURI TATU”

Kiini cha mpango huo ni ajenda ya “Sifuri Tatu”, inayolenga:

...Sifuri kwa vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga;

..Sifuri kwa kujifungua katika mazingira yasiyo salama na rufaa zisizo na huduma stahiki;

..Sifuri kwa watoto ambao hawajapata chanjo.

Ajenda hiyo inazitaka Serikali za Afrika, jamii, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi kuongeza kasi ya utekelezaji badala ya kubaki kwenye ahadi.

Rais Samia aliteuliwa kuwa Kinara wa AU katika Afya ya Mama na Mtoto katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Februari 2026.

Uteuzi huo unampa Tanzania nafasi ya kuongoza juhudi za bara katika kuimarisha afya ya uzazi, kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga na kuhakikisha watoto wanapata huduma muhimu za kinga na matibabu.

Arusha Septemba 9 inatarajiwa kuwa jukwaa la kuweka mwelekeo wa Afrika wa miaka mitano ijayo katika mapambano ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post