Ad
Breaking🔥

MKUDE AONGOZA USAFI KILOMBERO, ATOA TAHADHARI MVUA KUBWA

MKUDE AONGOZA USAFI KILOMBERO, ATOA TAHADHARI MVUA KUBWA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA



MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewaongoza wananchi na viongozi mbalimbali kufanya usafi katika Soko la Kilombero jijini Arusha, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya uwezekano wa mvua kubwa za El Niño.

Zoezi hilo lililofanyika jana, Septemba 19, 2026, ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuendelea kuimarisha usafi na usalama wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.




Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Mkude alisema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema kwa kusafisha mitaro, mifereji na maeneo mengine yanayoweza kuziba na kusababisha maji kushindwa kupita, hali inayoweza kuongeza hatari ya mafuriko.

Aliwataka wananchi kutobweteka, bali kuhakikisha taka hazitupwi kwenye mitaro na mifereji ya maji, akisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kupunguza athari zinazoweza kujitokeza endapo mvua kubwa zitanyesha.

“Ni muhimu kila mmoja wetu kuchukua tahadhari na kuhakikisha mitaro na mifereji inakuwa wazi ili maji ya mvua yaweze kupita bila kusababisha mafuriko,” alisema Mkude.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alizitaka taasisi mbalimbali kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kuokoa maisha na mali za wananchi.

Mkude pia aliwashukuru madiwani, viongozi mbalimbali na wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo, akisema usafi wa mazingira hauwezi kuwa jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushiriki wa kila mwananchi.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha Jiji la Arusha linabaki katika hali ya usafi, huku mazingira yakilindwa na afya za wananchi zikizingatiwa.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post