TEKNOLOJIA YA MIZINGA YA NYUKI YA PLASTIKI YAZINDULIWA MEATU
Na Mwandishi Wetu|ArushaDigital|MEATU
TAASISI ya Friedkin Conservation Fund (FCF) imeanza majaribio ya matumizi ya mizinga ya nyuki iliyotengenezwa kwa plastiki, teknolojia inayolenga kuongeza uzalishaji wa asali huku ikisaidia kulinda mazingira katika Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu.
Mizinga hiyo inayotoka nchini Uturuki, inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa asali hadi mara tatu zaidi ikilinganishwa na mizinga ya kawaida inayotengenezwa kwa mbao, miti na mabati.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya uwezeshaji na maendeleo ya jamii ya Friedkin Conservation Fund na Mwiba Holdings Ltd katika Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (AZAKI) Wilaya ya Meatu, Afisa Mafunzo ya Ufugaji Nyuki wa FCF, Baraka Mabula, alisema tayari wameanza kufanya majaribio kwa kuweka makundi ya nyuki katika mizinga hiyo.Alisema teknolojia hiyo inalenga kubadilisha baadhi ya taratibu za ufugaji na uvunaji wa asali, ikiwemo kuachana na matumizi ya moto wakati wa kuvuna, jambo linaloweza kuathiri makundi ya nyuki na mazingira.
“Tumianza majaribio na tayari makundi ya nyuki yameanza kuingia katika mizinga hii. Tukiona ufanisi mkubwa, tutaanza kuwagawia wafugaji,” alisema Mabula.Alisema mizinga hiyo imeundwa kwa mfumo unaosaidia kudhibiti joto ndani ya mzinga, huku ikiwa na masega maalumu ambayo nyuki hutumia kuhifadhi asali.
Kwa mujibu wa Mabula, mfumo huo pia unamwezesha mfugaji kuvuna asali bila kuwaathiri nyuki, hivyo kuongeza uwezekano wa kuvuna zaidi ya mara moja kwa mwaka.
“Teknolojia hii itasaidia kuzuia utaratibu wa kutumia moto wakati wa uvunaji wa asali, huku mfugaji akiwa na uwezo wa kurina asali mara tatu kwa mwaka,” alisema.
VIKUNDI 16 VYAWEZESHWA
Akizungumzia programu za ufugaji nyuki zinazotekelezwa na FCF, Mabula alisema mwaka 2026 taasisi hiyo imewezesha zaidi ya vikundi 16 vya wafugaji nyuki.
Alisema vikundi hivyo vina jumla ya wanachama 699, wakiwemo wanaume 119 na wanawake 244, huku vikundi hivyo vikiwa tayari vimeanza kunufaika na shughuli za ufugaji nyuki.
“Msimu wa mwaka 2025/2026, jumla ya tani 4.27 za asali zilivunwa,” alisema.
WANAFUNZI WAFUNDISHWA ELIMU YA MAZINGIRA
Katika mpango wa stadi za maisha na elimu ya mazingira mashuleni, Mabula alisema wanafunzi 4,822 wanaoshiriki katika klabu za shule wamepatiwa elimu ya mazingira.
Alisema kati yao, wavulana ni 2,394 na wasichana 2,428.
Aidha, alisema wanafunzi 2,445 wamepatiwa mafunzo ya stadi za maisha, ambapo wavulana ni 775 na wasichana 1,670.
MEATU YAPONDA TEKNOLOJIA
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Protas Dibogo, aliipongeza FCF kwa kuanzisha majaribio ya teknolojia hiyo ya mizinga ya plastiki, akisema ina uwezo wa kuongeza tija katika ufugaji nyuki.
Friedkin Conservation Fund (FCF) ni taasisi inayotekeleza shughuli za kijamii kwa niaba ya Mwiba Holdings Ltd katika jamii zinazozunguka Pori la Akiba la Maswa, ikilenga kusaidia maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira.
Ends


Post a Comment