LUKUMAY ATOA AHADI NZITO NDURUMA
......Aahidi kuibeba kero ya maji hadi Bungeni, atangaza maboresho ya barabara, afya na umeme
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameahidi kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Kata ya Nduruma wilayani Arumeru, akisisitiza kuwa suala la maji, ambalo limekuwa kilio kikuu cha wakazi wa eneo hilo, atalifikisha hadi Bungeni ili kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Katika ziara yake ya kutembelea, kukagua na kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo, Dkt. Lukumay aliahidi kushirikiana na Serikali na wataalamu wa halmashauri katika kutekeleza ahadi zilizotolewa, huku akitangaza pia kutumia fedha zake binafsi kugharamia mafunzo ya waendesha bodaboda na masomo ya kijana mwenye kipaji cha kuchora.“Yale ambayo tumetoa ahadi tuyatekeleze. Hawa wananchi hawana shida, wanataka maendeleo. Ni watu wasikivu, wana imani kubwa sana na Serikali yao, tena wana imani na mbunge wao,” alisema.
MAJI KUPEWA KIPAUMBELE, KERO KUFIKISHWA BUNGENI
Dkt. Lukumay alisema maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Nduruma, akiahidi kulifuatilia kwa karibu na kulifikisha Bungeni ili kupata ufumbuzi.
Alisema atashirikiana na wataalamu wa maji, mamlaka husika na viongozi wa Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu, huku akisisitiza umuhimu wa kupeleka maji katika Kituo cha Afya Nduruma.
“Suala kubwa sana ni maji. Tunataka maji yapatikane katika kituo cha afya. Tutafuatilia hili kwa sababu wananchi wanahitaji huduma nzuri ya afya,” alisema.
BARABARA YA LAMI KUFIKIA KILOMITA 27
Katika eneo la miundombinu, mbunge huyo alisema juhudi zinaendelea kuboresha barabara ya lami inayohudumia eneo hilo, akieleza kuwa mpango uliopo ni kuifanya ifikie kilomita 27 badala ya kilomita tano zilizokuwa zimepangwa awali.
Dkt. Lukumay pia alisema amewasilisha hoja ya kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) hadi Sh bilioni sita kwa mwaka, akieleza kuwa ongezeko hilo litasaidia kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo hilo.
“Barabara yetu ya lami inaendelea. Nimeomba bajeti ya TARURA ifike bilioni sita kwa mwaka. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza pia bajeti ya TARURA, kwa hiyo tusubiri kwa sababu bajeti inaanza na barabara hii itatengenezwa,” alisema.
Aliongeza kuwa amezungumza na Waziri wa Mipango na Uwekezaji kuhusu uwezekano wa kuboresha barabara ya lami kutoka eneo la mashamba ya maua kuelekea Nduruma, akisema hatua hiyo itarahisisha usafirishaji wa mazao na kuchochea shughuli za kiuchumi.
AFYA: DAWA, VIFAA TIBA NA WODI KUONGEZWA
Akizungumzia huduma za afya, Dkt. Lukumay alisema Kituo cha Afya Nduruma kinahitaji kuimarishwa ili kiweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Alitaja upatikanaji wa dawa kwa wakati, vifaa tiba na upanuzi wa wodi kuwa miongoni mwa mahitaji yanayopaswa kupewa kipaumbele, akiahidi kushirikiana na halmashauri pamoja na wataalamu wa afya katika kufuatilia utekelezaji wake.
“Dawa zipatikane kwa wakati wote, vifaa tiba vipatikane na tuongeze wodi, tupanuie kituo hiki kwa sababu wananchi wa Nduruma wanahitaji huduma nzuri ya afya,” alisema.
BODABODA WAPATA AHADI YA MAFUNZO NA SH MILIONI MOJA
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alitangaza kugharamia mafunzo ya waendesha bodaboda kwa fedha zake binafsi, akisema lengo ni kuwawezesha kuzingatia usalama barabarani, matumizi ya kofia ngumu na uendeshaji salama wa pikipiki.
Alimtaka Mkuu wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC) kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda wa Nduruma.
“Kwa mafunzo, mimi nitagharamia kwa fedha zangu binafsi. Naomba RPC afanye utaratibu wa kuja kuwapatia mafunzo watu wa bodaboda, pamoja na kuvaa kofia ngumu na kutokimbiza pikipiki kwa kuhatarisha maisha ya watu,” alisema.
Mbunge huyo pia aliahidi kutoa Sh milioni moja kwa waendesha bodaboda, akisisitiza kuwa fedha hizo zitatolewa kutoka katika fedha zake binafsi, siyo bajeti ya Bunge.
VITONGOJI 48 VYALENGWA KUPATIWA UMEME
Kuhusu umeme, Dkt. Lukumay alisema jimbo hilo lina vitongoji 48 ambavyo havikuwa na huduma hiyo, huku akieleza kuwa juhudi zimefanyika kupitia bajeti ya Serikali ili kuhakikisha vinapatiwa umeme.
Alisema vitongoji sita bado vinahitaji ufuatiliaji zaidi, akiwataka wananchi wenye changamoto za umeme kuwasilisha taarifa zao kwa viongozi wa maeneo yao ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Tunapigania ili vitongoji vyote vipate umeme. Hii ni haki yenu, na tutaendelea kupambana kuhakikisha wananchi wa jimbo hili wanapata huduma hiyo,” alisema.
KIJANA MWENYE KIPAJI APEWA AHADI YA MASOMO
Katika tukio lililovuta hisia za wananchi, Dkt. Lukumay aliahidi kumlipia masomo kijana mmoja wa Nduruma aliyemkabidhi zawadi ya mchoro, akisema amevutiwa na kipaji chake na anataka kukisaidia kikue.
Mbunge huyo alisema yuko tayari kugharamia masomo ya kijana huyo katika chuo au taasisi itakayosaidia kukuza kipaji chake, akisisitiza kuwa msaada huo utatolewa kwa fedha zake binafsi.
“Nitakulipia usome, uimarishe taaluma yako. Umeonyesha kipaji kikubwa na unaweza kufanya makubwa zaidi kitaifa. Mimi na wewe, unataka nini? Nitakulipia,” alisema.
Ahadi hiyo imeongeza msisitizo kuhusu umuhimu wa kutambua na kuendeleza vipaji vya vijana katika jamii, huku Dkt. Lukumay akiwashukuru wananchi kwa kuibua vipaji vya vijana wao na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo katika Kata ya Nduruma.
Ends




إرسال تعليق