Breaking🔥

LUKUMAY AINGIA KATI KERO YA MAJI NDURUMA, WANANCHI WADAI WANAKAA HADI WIKI MBILI BILA HUDUMA HIYO

 LUKUMAY AINGIA KATI KERO YA MAJI NDURUMA, WANANCHI WADAI WANAKAA HADI WIKI MBILI BILA HUDUMA HIYO

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU 

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, amewataka viongozi na wataalamu wa maji kuongeza kasi ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Nduruma, baada ya wananchi kulalamikia kukaa hadi wiki mbili bila kupata huduma hiyo.

Wananchi hao pia wameilalamikia Mamlaka ya Watumia Maji ya Mlangarini, Bwawani na Nduruma (MLABWANDU), wakidai kuwa licha ya kuwa chombo kinachohusika na huduma ya maji katika kata hizo, bado hawapati huduma ya uhakika.

Malalamiko hayo yalitolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Marurani na Nduruma, Kata ya Nduruma, wakati Dkt Lukumay alipokuwa akisikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Wananchi walisema changamoto ya maji imekuwa ikiwalazimu kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo, huku baadhi yao wakidai kuwa hukaa muda mrefu bila maji.

Walisema hali hiyo imekuwa ikiwaletea usumbufu katika shughuli za kila siku, zikiwamo matumizi ya majumbani na shughuli nyingine za kiuchumi.

Wakizungumzia MLABWANDU, wananchi walitaka chombo hicho kusikiliza zaidi changamoto zao na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia kwa wakati, badala ya kuwaacha wakisubiri kwa muda mrefu.

Akijibu kero hiyo, Dkt Lukumay alisema suala la maji ni miongoni mwa vipaumbele vyake katika Jimbo la Arumeru Magharibi na kwamba aliahidi kulipatia uzito wa aina yake suala hilo ikiwemo kulifikisha bungeni na kuonana na waziri mwenye dhamana.

Alisisitiza wataalamu wanapaswa kwenda kwa wananchi ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema wananchi wanapokuwa na changamoto ya maji, wanapaswa kupewa majibu ya wazi kuhusu tatizo lilipo, gharama zinazohitajika na hatua zinazochukuliwa kulitatua.

“Kama mwananchi anasema anahitaji maji, msikilize. Kama kuna gharama au utaratibu unaotakiwa kufuatwa, mweleze. Mwananchi akielezwa anaelewa, lakini tatizo ni pale ambapo haelezwi kinachoendelea,” alisema.

Dkt Lukumay pia aliwataka wataalamu wa maji kushirikiana na viongozi wa maeneo husika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinabainishwa na kutatuliwa kwa wakati.

“Wasikilize wananchi. Wana wananchi wana shida, hata kidogo. Kama kuna tatizo, lielezeni na tulitafutie ufumbuzi. Maji ni kipaumbele changu na nitaendelea kulifuatilia,” alisema.

Alisema viongozi na wataalamu hawapaswi kusubiri wananchi wawafuate ofisini, bali wanapaswa kufika katika maeneo yao, kuona changamoto wanazokabiliana nazo na kuchukua hatua.

Dkt Lukumay alisema uwepo wa Serikali na taasisi zinazohusika na huduma za maji unapaswa kuonekana kupitia huduma inayowafikia wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuwajibika kwa wananchi wanaotegemea huduma hiyo.

“Tunachohitaji sasa si maneno mengi, bali kazi, kasi, uwajibikaji na matokeo,” alisema.

Kero ya maji imekuwa miongoni mwa changamoto zilizotawala mkutano huo, huku wananchi wakitaka hatua zichukuliwe kuhakikisha wanapata huduma ya uhakika badala ya kukaa muda mrefu bila maji.


Ends

Post a Comment

أحدث أقدم