LISSU :DCI KINGAI ASEMA HAYUKO TAYARI KUTOA USHAHIDI WA UTETEZI
DAR ES SALAAM:By Arushadigutal
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kwamba Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, amemweleza kuwa hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili.Lissu ameyasema hayo wakati akiendelea na hatua ya ushahidi wa upande wa utetezi mbele ya Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akieleza kuwa ameshafanya mawasiliano na DCI Kingai kuhusu maeneo aliyokusudia kumhoji iwapo angefika mahakamani kutoa ushahidi.
Kwa mujibu wa Lissu, katika mazungumzo yao, Kingai alimweleza kuwa hayuko tayari kutoa ushahidi katika shauri hilo, hali ambayo, kwa mujibu wa Lissu, imemweka katika mazingira ya kutokuwa na uwezo wa kuwalazimisha mashahidi hao kutoa ushahidi kwa upande wake.
Lissu amedai zaidi kwamba DCI Kingai alimweleza kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura, nao wanaweza kuwa na msimamo kama huo watakaporejea nchini.
Hatua hiyo imeibuka baada ya Mahakama Kuu, Septemba 10, 2026, kuridhia ombi la Lissu la kuwaita Kingai, Mkunda na Wambura kuwa mashahidi wa upande wa utetezi katika kesi hiyo. Mahakama, hata hivyo, ilikataa ombi la kuwaita baadhi ya mashahidi wengine waliotajwa na Lissu.
Akieleza msimamo wake mbele ya Mahakama, Lissu amesema kutokana na maelezo aliyoyapata kutoka kwa DCI Kingai, hana nia ya kuendelea kusubiri mashahidi hao iwapo hawako tayari kufika kutoa ushahidi.
Kwa msingi huo, Lissu ameomba Mahakama imruhusu kufunga ushahidi wa upande wa utetezi, akieleza kuwa hawezi kuwalazimisha mashahidi aliowataka kutoa ushahidi dhidi ya utashi wao.
Aidha, Lissu ameomba Mahakama ipange utaratibu wa kusikiliza hoja za mwisho za pande zote mbili, akipendekeza hoja hizo zitolewe kwa njia ya mdomo.
Amesema ombi hilo linatokana na mazingira aliyonayo akiwa mahabusu, akieleza kuwa hana zana na mazingira yanayomwezesha kuandaa hoja hizo kwa maandishi kwa namna anayohitaji.
Kesi hiyo imefikia hatua muhimu baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi wake kupitia mashahidi kadhaa. Kabla ya hatua hii, Mahakama ilikuwa imeridhia mashahidi watatu kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama kuitwa kwa ajili ya upande wa utetezi, huku DCI Kingai akitarajiwa kuwa miongoni mwa mashahidi hao.
Kwa upande wake, Mahakama imepanga shauri hilo kuendelea Jumatano, Septemba 23, 2026, ambapo hoja za mwisho za pande zinazohusika zinatarajiwa kusikilizwa kwa njia ya mdomo.
Kesi hiyo ya uhaini, yenye namba 19605/2025, ni shauri la jinai linalomkabili Lissu na limekuwa likisikilizwa mbele ya Jopo la Majaji watatu chini ya uongozi wa Jaji Dunstan Ndunguru.
#ArushaDigitalUPDATES
إرسال تعليق