Breaking🔥

BATULI AIBUA SIRI NZITO YA MAFANIKIO YA DEUS MIHAMBO NI BAADA YA TUZO, AMFANYIA BONGE LA SURPRISE

BATULI AMPONGEZA MUMEWE DEUS MIHAMBO KWA BONGE LA SURPRISE ,NI BAADA YA KUSHINDA TUZO NZITO

...ATOBOA SIRI NZITO YA MIAKA 20 NYUMA YA DEUS MIHAMBO

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MWALIMU Batuli Kisaya, mke wa msanii wa filamu nchini, Deus Mihambo, amefichua siri ya safari ya zaidi ya miaka 20 ya ndoa yao, akisema amekuwa bega kwa bega na mumewe katika vipindi vya mafanikio na changamoto, huku ushindi wa tuzo ya Best Actor – People’s Choice 2026 ukimpa sababu mpya ya kumshangilia
Batuli aliyasema hayo katika hafla maalum ya chakula na zawadi aliyomwandalia mumewe baada ya kutwaa tuzo hiyo ya Kigamboni Awards, katika ushindi uliotokana na kura za mashabiki na jamii.

Hafla hiyo iliyowakutanisha ndugu, jamaa, marafiki na majirani, iligeuka kuwa sherehe ya kumpongeza Mihambo kwa hatua hiyo kubwa katika safari yake ya sanaa, huku akipewa zawadi mbalimbali kama ishara ya kutambua mchango wake katika tasnia ya filamu.



Batuli alisema aliamua kumfanyia mumewe surprise hiyo baada ya kuona kuwa ushindi huo ulipaswa kusherehekewa kwa namna ya kipekee.

“Niliona nitafute sehemu ambayo inaweza kumpokea vizuri. Nikaandaa lunch na surprise kidogo, nikawashirikisha baadhi ya marafiki na majirani. Lengo langu lilikuwa kumpongeza na kumtia moyo,” alisema.

MIAKA 20 YA NDOA YA USHINDI NA CHANGAMOTO


Akizungumzia nafasi yake katika safari ya Mihambo, Batuli alisema licha ya kutokuwa msanii, amekuwa mmoja wa watu muhimu waliomsimamia mumewe katika kutimiza ndoto zake za kisanii.

Alisema kwa zaidi ya miaka 20 ya ndoa yao, amekuwa akimpa moyo, ushauri na nafasi ya kuendelea kuamini katika kipaji chake hata katika nyakati ambazo mambo hayakuwa rahisi.

“Yeye ni msanii, mimi si msanii, lakini niko nyuma yake kama mama, rafiki na mke. Kwa miaka 20 ya ndoa yetu nimekuwa nikimtia moyo aendelee kujitafuta na kufuata ndoto zake,” alisema.

Batuli alisema siri nyingine ya kudumu kwao ni kuaminiana, kuheshimiana na kushirikishana mambo yanayohusu familia, ikiwamo malezi ya watoto.

“Hatujajenga ndoa kwa changamoto. Tuna utaratibu wa kuheshimiana, kushirikishana mipango ya familia na mambo ya watoto. Tunapeana uhuru lakini ndani ya mipaka na kanuni za familia,” alisema.

Hata hivyo, alisema kama ilivyo kwa familia nyingine, changamoto zipo, akitaja kutopenda baadhi ya picha za mumewe akiwa katika mazingira ya kikazi na wanawake pale anapoona mazingira hayo hayaeleweki.

Pamoja na hilo, alisema msingi wa uhusiano wao ni imani na kumfahamu mumewe kama mtu anayejua mipaka na maadili ya familia.

“TUZO HII NI HESHIMA KUBWA”



Batuli alisema ushindi wa Mihambo ni uthibitisho kwamba kazi yake imeanza kutambuliwa na kuthaminiwa na mashabiki.

“Kwa kweli nimefurahi sana kwa sababu kupata tuzo kama hii si jambo dogo. Kuna juhudi binafsi, kuna kipaji, lakini pia kuna watu wamemuona na wakaamua kumpigia kura,” alisema.

Kwa upande wake, Mihambo alisema ushindi huo umempa nguvu mpya na anauchukulia kama mwanzo wa hatua nyingine katika maisha yake ya kisanii.

Alisema alishindana na wasanii wenye majina makubwa, akiwamo Gabo Zigamba, Madebe  maarufu Nabii Mswahili, Babahaji maarufu Adi Adam na Kazoa, lakini kura za mashabiki zikampa ushindi.

“Kwa kweli hii tuzo haikuwa rahisi. Tulikuwa tunagombea na wasanii ambao wamefanya sanaa kwa muda mrefu na wana majina makubwa. Kwangu hii ni heshima kubwa na mwanzo mpya,” alisema.

Mihambo alisema aliteuliwa kuwania tuzo hiyo na kampuni ya Mroni Twins, inayomilikiwa na mapacha Regina na Christina, kutokana na nafasi yake katika filamu Panya Wajinga.

“Sikuwa mimi niliyeomba kugombea. Mroni Twins waliona ninastahili kuwepo kwenye kinyang’anyiro. Wakanipendekeza na hatimaye nimepata tuzo. Nawashukuru sana kwa kuniamini,” alisema.

“NIMEANZA UPYA KWA NGUVU”


Msanii huyo alisema tuzo hiyo haimpi nafasi ya kujivuna, bali inamuongezea wajibu wa kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuthibitisha kuwa ushindi huo umetokana na uwezo na kazi yake.

“Tuzo hii imenistart upya. Naanza tena kwa nguvu kubwa. Natakiwa kufanya kazi zaidi ili hata wale ambao hawakuwa wananijua waseme kweli Mihambo anastahili tuzo hii,” alisema.

Akizungumzia falsafa yake katika kujenga jina kwenye tasnia, Mihambo alisema hataki kutumia skendo kama njia ya kutafuta umaarufu, akisisitiza kuwa anataka kutambulika kupitia kazi na maadili.

“Mimi siyo msanii wa skendo. Nataka nijulikane kwa kazi yangu. Nimelelewa katika maadili na najua ninachotakiwa kufanya na nisichotakiwa kufanya,” alisema.

BATULI: “ONGEZA BIDII”

Batuli naye hakusita kumpa mumewe kazi ya kufanya baada ya ushindi huo, akimtaka kuongeza ubunifu na uhalisia katika uigizaji ili kuwafanya mashabiki waone tofauti katika kazi zake.

“Cha kwanza aongeze bidii, cha pili afanye kazi kwa ufanisi. Ukiwa kwenye scene ya kulia, lia kwa uhalisia; ukiwa kwenye scene ya kucheka, cheka kwa uhalisia. Mashabiki wanapotazama wanapaswa kuona kipaji chako na kuhisi kile unachokifanya,” alisema.

Alisema ataendelea kuwa nyuma ya Mihambo katika safari yake ya sanaa, huku akimtaka kutumia ushindi huo kama chachu ya kufungua ukurasa mpya wa mafanikio.

Kwa upande wake, Mihambo amewaomba mashabiki kuendelea kumuunga mkono, akisema ushindi huo umempa kiu ya kufanya kazi kubwa zaidi na kuongeza ubora wa kazi zake.

Baadhi ya kazi zake zinapatikana kupitia Mihambo Film kwenye YouTube, huku msanii huyo akiahidi kuendelea kuwafikia mashabiki kwa kazi mpya baada ya kupata nguvu mpya kutokana na tuzo hiyo.











Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post