Breaking🔥

WEST KILIMANJARO RANCHING YAANZA MAPINDUZI YA UFUGAJI KWA KITUO CHA KISASA CHA MBEGU ZA MIFUGO YAWEKEZA BILIONI 15




Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KAMPUNI ya West Kilimanjaro Ranching imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuboresha vinasaba vya mifugo nchini kwa kujenga kituo cha kisasa cha uzalishaji wa mbegu za uzazi (semen) na embryo, uwekezaji unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbegu bora za mifugo Afrika Mashariki.


Kupitia uwekezaji huo, kampuni imeanza kuingiza mifugo bora kutoka Kenya, Namibia na Afrika Kusini, kuizoesha katika mazingira ya Tanzania na kuzalisha mbegu zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa pamoja na kuinua kipato cha wafugaji.


Akiongea katika maonesho ya wakulima Nane kanda ya kaskazini yaliyopo Njiro Jijini Arusha,Mkurugenzi wa West Kilimanjaro Ranching, Mirzad Akram Aziz, alisema matumizi ya mbegu bora na teknolojia za kisasa ndiyo msingi wa mapinduzi ya sekta ya mifugo nchini.


"Tunataka kuona wafugaji wa Tanzania wanapata mifugo yenye tija, inayostahimili mazingira yetu na inayoongeza uzalishaji wa nyama na maziwa. Dhamira yetu ni kuifanya Tanzania ijitosheleze kwa mbegu bora za mifugo na kuwa kitovu cha huduma hizi katika Afrika Mashariki," alisema Aziz.


Alisema kampuni hiyo inayofanya shughuli zake katika shamba la hekta 2,500 lililopo West Kilimanjaro, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, eneo ililokabidhiwa na Shirika la Taifa la Ranchi (NARCO), inaendelea kujenga kituo cha kisasa cha uzalishaji wa embryo na mbegu za uzazi (Semen Centre) kitakachopunguza utegemezi wa huduma hizo kutoka nje ya nchi.


Aziz alisema pamoja na uwekezaji huo, kampuni imeendelea kushiriki katika maonesho ya mifugo nchini kwa lengo la kuwahamasisha wafugaji kutumia mbegu bora na teknolojia za kisasa za uzazi ili kuongeza tija ya mifugo.


Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Mradi wa kampuni hiyo, Adil Butt, alisema West Kilimanjaro Ranching inafuga ng'ombe wa aina za Boran, Simmental, Tuli na ng'ombe wa asili wanaotumika katika programu za kuboresha vinasaba.


Alisema kampuni pia inafuga kondoo wa aina za Meatmaster, Dorper na Red Maasai, huku ikiwa imeingiza Persian Blackhead kutoka Namibia ili kuongeza vinasaba vipya na kupunguza tatizo la kuzaliana kwa ndugu (inbreeding), ambalo limekuwa likijitokeza kutokana na kutokuingizwa kwa uzao huo nchini kwa zaidi ya miaka 50.


"Malengo yetu ni kuwafikishia wafugaji wa Tanzania mbegu bora zitakazoongeza uzalishaji, tija na kipato kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji," alisema Butt.


Alisema kampuni inaendesha programu maalumu ya kuboresha vinasaba kwa kushirikiana na vikundi vya wafugaji vitakavyosajiliwa rasmi na kupatiwa mbegu bora pamoja na huduma za kitaalamu za uzazi wa mifugo.


Kwa mujibu wa Butt, tangu kampuni ilipoanza shughuli zake mwaka 2024, idadi ya ng'ombe imeongezeka kutoka 700 hadi 1,200, huku mbuzi na kondoo wakiongezeka kutoka 2,000 hadi karibu 4,000.


Mbali na uwekezaji katika mifugo, kampuni imeendelea kushirikiana na jamii kupitia utekelezaji wa miradi ya maji, afya, elimu, miundombinu na ajira.


Afisa Mahusiano wa kampuni hiyo, Lee Mamasita, alisema West Kilimanjaro Ranching inashirikiana na zaidi ya vijiji 10 vya wilaya za Siha, Longido na Rombo, ambapo imechimba mabwawa mawili ya maji katika eneo la Tingatinga, kusambaza lita 20,000 za maji bure kila wiki kwa shule na zahanati ya Ngerejani, kuchangia vifaa vya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na kujenga barabara ya kilomita tatu kuelekea Tingatinga.


Alisema kampuni imeajiri zaidi ya watu 210, wakiwemo 188 kutoka katika jamii zinazozunguka ranchi hiyo, huku wanawake 62 wakishiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.


Aidha, kampuni imenunua mamia ya ng'ombe, mbuzi na kondoo wa asili kutoka kwa wafugaji wa Engaruka, Monduli na Morogoro, hatua iliyowaongezea kipato wafugaji na kuchochea biashara ya mifugo nchini.


Kwa mujibu wa West Kilimanjaro Ranching, uwekezaji huo unalenga kuongeza tija ya uzalishaji wa mifugo, kufungua ajira, kuinua kipato cha wafugaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbegu bora za mifugo katika Afrika Mashariki.


Ends..


Post a Comment

Previous Post Next Post