WATOTO WA MIAKA MIWILI WATAKIWA KUPELEKWA VITUO VYA MALEZI
Na Hadija Bagasha | TANGA
Wito huo umetolewa kutokana na hali ya ukuaji wa watoto nchini, ambapo utafiti unaonyesha kuwa ni asilimia 47 pekee ya watoto wanaofikia kiwango cha ukuaji timilifu, huku Mkoa wa Tanga ukiwa na changamoto zaidi, ambapo asilimia 46 ya watoto hawafikii kiwango hicho.
Kutokana na hali hiyo, wadau kupitia Mradi wa Tanga Yetu wameanzisha mpango wa kuongeza fursa za huduma za malezi, makuzi na ujifunzaji wa awali, hususan kwa watoto wenye umri wa miaka miwili hadi mitano ambao wengi wao hubaki nyumbani bila kupata huduma hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Dkt. Samweli Mtulu kutoka Mradi wa Maendeleo ya Awali ya Mtoto, alisema lengo la mpango huo ni kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama na rafiki ya kujifunza, kucheza na kuendeleza uwezo wao tangu wakiwa wadogo.
Alisema mpango huo unalenga pia kuimarisha ushiriki wa jamii katika malezi ya watoto, hasa katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji ambako huduma za malezi na ujifunzaji wa awali bado hazijawafikia watoto wengi.“Watoto wengi wanabaki majumbani kuanzia umri wa miaka miwili mpaka mitano, wakati huo ni kipindi muhimu sana ambacho ubongo wa mtoto unatakiwa ukue vizuri. Hivyo, kunakuwa na upungufu wa huduma za malezi na ujifunzaji wa awali,” alisema Dkt. Mtulu.
Alisema Serikali tayari imetambua umuhimu wa malezi na makuzi ya awali na imeweka mwongozo wa kuanzishwa kwa vituo vya malezi ya watoto wadogo, hatua ambayo inalenga kuhakikisha watoto wanapata huduma muhimu kabla ya kuanza elimu ya msingi.
Dkt. Mtulu alisema changamoto nyingine imebainika katika Jiji la Tanga, ambapo utafiti umeonyesha kuwa ni asilimia 40 pekee ya watoto wanaoingia darasa la kwanza waliowahi kupata elimu ya awali, maarufu kama chekechea, huku asilimia 60 wakiwa hawajawahi kupitia elimu hiyo.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kuongeza jitihada za kuhakikisha watoto wanapata huduma za malezi, makuzi na ujifunzaji wa awali kabla ya kuanza darasa la kwanza.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, alisema wadau kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga wamefanikiwa kuanzisha vituo tisa katika maeneo ya pembezoni mwa jiji, vinavyotoa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, ikiwemo ujifunzaji.
“Ushiriki wa jamii ni muhimu kwa sababu sehemu kubwa ya watoto wanaohitaji huduma hizi wanaishi katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji. Kwa hiyo, kuanzisha vituo vinavyoendeshwa kwa ushirikiano na jamii kutasaidia kuwafikia watoto wengi zaidi,” alisema.
Alisema vituo hivyo vina umuhimu mkubwa kwa kuwa vinatoa nafasi kwa watoto kujifunza kupitia michezo na shughuli mbalimbali zinazowasaidia kukuza uwezo wa kufikiri, kuwasiliana na kushirikiana na wenzao.
Mradi huo wa kuanzisha vituo vya kulelea watoto wenye umri kuanzia miaka miwili ni sehemu ya Mradi wa Tanga Yetu, unaofadhiliwa na Botner Foundation kupitia kampuni ya Innovex.
Dkt. Mtulu alisisitiza kuwa maendeleo ya mtoto hayawezi kutenganishwa na huduma za afya, lishe, malezi bora na ujifunzaji, akisema uwekezaji katika maeneo hayo tangu mtoto akiwa mdogo una mchango mkubwa katika maisha yake ya baadaye.
Alisema hatua hiyo pia itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaoanza darasa la kwanza bila kuwa na uzoefu wa elimu ya awali, hali ambayo inaweza kuathiri uwezo wao wa kuendana na mazingira ya shule.
Kwa mujibu wa Dkt. Mtulu, mafanikio ya mpango huo yatategemea ushirikiano wa Serikali, wazazi, walezi, jamii na wadau wa maendeleo kuhakikisha vituo vinaanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia mahitaji ya watoto.
Alisema lengo la muda mrefu ni kuongeza idadi ya watoto wanaofikia ukuaji timilifu na kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujenga msingi imara wa maendeleo ya kielimu, kiafya na kijamii tangu akiwa katika hatua za awali za maisha.



إرسال تعليق