TANAPA YATAKIWA KUKIMBIZA UKARABATI WA BARABARA ZA HIFADHI
Na Joseph Ngilisho | DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeitaka Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kuharakisha ukarabati na uboreshaji wa barabara ndani ya hifadhi za taifa kabla ya kuanza kwa mvua za vuli.
Kamati hiyo imesema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda shughuli za utalii, kurahisisha shughuli za uhifadhi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori dhidi ya changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua.
Maelekezo hayo yametolewa jana, Agosti 20, 2026, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava, wakati kamati ilipopokea taarifa ya utendaji wa TANAPA katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
Mnzava amesema ubora wa barabara ndani ya hifadhi ni sehemu muhimu ya miundombinu ya utalii, kwa kuwa huwawezesha watalii kufika katika maeneo yenye vivutio kwa urahisi na kupata huduma bora wakati wa ziara zao.
Amesema barabara hizo pia ni muhimu kwa shughuli za uhifadhi, kwani huwawezesha watendaji kufika kwa wakati katika maeneo mbalimbali ya hifadhi kwa ajili ya doria, ufuatiliaji na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori.
“Tunaitaka TANAPA kuendelea kuimarisha na kuboresha miundombinu ya hifadhi kwa kuweka kipaumbele katika miundombinu ya barabara ili kuepukana na changamoto zinazosababishwa na mvua za vuli ambazo zinaweza kuharibu miundombinu hiyo,” amesema Mnzava.
Amesema TANAPA inapaswa kuchukua hatua mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua, ambazo zinaweza kusababisha barabara kukatika au kuharibika na hivyo kuathiri usafirishaji wa watalii pamoja na shughuli za ulinzi wa hifadhi.
SERENGETI
Mbali na ukarabati wa barabara, Mnzava ameitaka TANAPA kuendelea kufanya utafiti wa teknolojia mbadala za ujenzi wa barabara katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Amesema utafiti huo unaweza kusaidia kupata teknolojia yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto ya barabara kuharibika mara kwa mara kutokana na mvua, hivyo kupunguza gharama za matengenezo na kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu kwa muda mrefu.
“Ni muhimu kuendelea kutafuta teknolojia mbadala, hasa katika maeneo kama Serengeti ambako changamoto ya barabara kuharibika kutokana na mvua imekuwa ikijitokeza mara kwa mara,” amesema.
KILOMITA 2,665.6
Maelekezo hayo ya Kamati yanakuja wakati Serikali kupitia TANAPA ikieleza kuwa imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya hifadhi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya TANAPA, shirika hilo limefanya matengenezo ya jumla ya kilomita 2,665.6 za barabara ndani ya hifadhi, pamoja na ukarabati wa kilomita 218.24 za njia za watembea kwa miguu.
Aidha, TANAPA imeendelea na ukarabati wa viwanja vya ndege nane, hatua inayolenga kuboresha usafiri na kurahisisha upatikanaji wa hifadhi kwa watalii na watendaji wa uhifadhi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha miundombinu ya hifadhi, kurahisisha shughuli za uhifadhi, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa maeneo hayo na kuboresha huduma kwa watalii.
Amesema kuimarishwa kwa miundombinu ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua sambamba na uhifadhi endelevu wa rasilimali za taifa.




إرسال تعليق