WANANCHI SYRIA WASHEREHEKEA HUKUMU YA KIFO KWA ALIYEKUWA RAIS WAO BASHAR AL-ASSAD
Na Joseph Ngilisho | Arushadigital
IDLIB, SYRIA — Wakazi wa mji wa Idlib nchini Syria wameingia mitaani kwa shamrashamra baada ya mahakama ya nchi hiyo kumhukumu kifo Rais wa zamani, Bashar al-Assad, katika hukumu inayofungua ukurasa mpya wa mchakato wa kuwawajibisha viongozi na maafisa wa utawala wake kwa madai ya uhalifu uliofanyika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mahakama ilimkuta Assad na hatia kwa makosa yanayohusishwa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, huku hukumu hiyo ikitolewa bila yeye kuwepo mahakamani.
Baada ya kutangazwa kwa hukumu hiyo, wakazi wa Idlib walionekana wakikusanyika katika maeneo mbalimbali ya mji wakishangilia. Picha na video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha baadhi ya wananchi wakipanda magari, kuimba na kusherehekea hatua hiyo ya mahakama.
Kwa wakazi wa maeneo yaliyokuwa ngome ya upinzani dhidi ya Assad, hukumu hiyo imeonekana kama hatua muhimu katika harakati za kutafuta haki kwa waathirika wa miaka mingi ya vita na ukandamizaji.
Assad aliondoka Syria na kukimbilia Urusi pamoja na familia yake baada ya utawala wake kuanguka mwezi Desemba 2024, hatua iliyohitimisha utawala wa familia ya Assad uliodumu kwa zaidi ya miongo mitano.
NAJIB NAYE AHUKUMIWA KIFO
Katika kesi hiyo hiyo, mahakama pia ilimhukumu kifo Atef Najib, binamu wa Assad na aliyekuwa mkuu wa usalama wa kisiasa katika jimbo la Deraa, kusini mwa Syria.
Tofauti na Assad, Najib alifika mahakamani na kuonekana akiwa ndani ya kizimba wakati jaji akisoma hukumu dhidi yake.
Deraa ina umuhimu mkubwa katika historia ya mzozo wa Syria, kwa kuwa eneo hilo linachukuliwa kuwa kitovu cha mwanzo wa maandamano yaliyopinga utawala wa Assad mwaka 2011.
KUKAMATWA KWA VIJANA KULIVYOCHOCHEA UASI
Mzozo huo ulianza Machi 2011 baada ya kundi la vijana kukamatwa na kudaiwa kuteswa kwa kuandika maandishi ya kupinga serikali kwenye kuta katika mji wa Deraa.
Hatua hiyo ilizua maandamano makubwa ambayo yalijibiwa kwa operesheni kali za vikosi vya usalama vya serikali.
Maandamano hayo yalienea katika maeneo mbalimbali ya Syria na hatimaye kubadilika kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka kadhaa, na kusababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu, huku mamilioni wengine wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
SERIKALI MPITO YAANZA MCHAKATO WA HAKI
Hukumu dhidi ya Assad na Najib inakuja wakati serikali ya mpito ya Syria ikiendelea na mchakato wa kuwafikisha mahakamani maafisa na watu wengine waliohusishwa na utawala wa zamani.
Serikali hiyo imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya maafisa wa utawala wa Assad, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushughulikia tuhuma za mauaji, mateso na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliojitokeza wakati wa vita.
Kwa wakazi wa Idlib, ambao kwa muda mrefu walikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa utawala wa Assad, hukumu hiyo imeibua hisia za ushindi na matumaini ya kuona wahusika wengine wanaodaiwa kuhusika na madhila ya vita wakifikishwa mbele ya sheria.
Hata hivyo, utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya Assad unaweza kuwa na changamoto kubwa kwa sababu yuko nje ya Syria, nchini Urusi, baada ya kupewa hifadhi kufuatia kuanguka kwa utawala wake.
Hivyo, hukumu hiyo inaweza kuwa mwanzo wa mvutano mpya wa kisheria na kidiplomasia kuhusu iwapo Moscow itamkabidhi Assad kwa mamlaka za Syria ili kukabili hukumu iliyotolewa dhidi yake.
Ends

Post a Comment