WANANCHI 8 WAMUOMBA RAIS ACHUNGUZE MGOGORO WA ARDHI ARUSHA
...Wadai makubaliano ya Huruma Vision yatekelezwe; Jiji lasitisha utekelezaji wa barua ya Juni 2025, lasema ekari zote tano zibaki kwa ajili ya shule
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
ARUSHA. Wananchi nane wa Kata ya Sokoni One, Jijini Arusha, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda timu maalumu ya uchunguzi kutoka Ikulu kuchunguza mgogoro wa ardhi wa Huruma Vision Tanzania, unaodaiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 14 na sasa kutishia kurejea mahakamani.
Wananchi hao, wakiongozwa na mwakilishi wao, Diwani mstaafu wa Kata ya Sokoni One, Michael Kivuyo, wanadai Halmashauri ya Jiji la Arusha imeshindwa kutekeleza makubaliano ya maandishi ya Juni 23, 2025, yaliyotokana na majadiliano ya kumaliza mgogoro huo nje ya mahakama.Kwa mujibu wa Kivuyo, makubaliano hayo yalihusisha eneo la jumla la ekari tano, ambapo ekari moja ilitengwa kwa ajili ya wananchi hao wanane na kila mmoja kuahidiwa Sh10 milioni kwa ajili ya gharama walizotumia katika mchakato wa kesi hiyo.
Hata hivyo, mvutano huo umechukua sura mpya baada ya Halmashauri ya Jiji kuwataka wahusika kutotekeleza maelekezo yaliyomo katika barua ya Juni 23, 2025, huku ikisema inaendelea na taratibu za kuifuta barua hiyo.
Badala yake, Halmashauri imesema ekari zote tano zibaki chini yake kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Hatua hiyo imeibua maswali mapya kutoka kwa wananchi hao ambao sasa wanataka Serikali Kuu iingilie kati na kuchunguza mchakato mzima, ikiwemo namna makubaliano yalivyofikiwa, kutengwa kwa ekari moja, malipo ya Sh10 milioni kwa kila mmoja na sababu za kubadilishwa kwa msimamo wa Halmashauri.
MAKUBALIANO YA JUNI 23
Kivuyo amesema madai yao hayahusu makubaliano mapya wala upendeleo, bali utekelezaji wa kile anachodai kiliandikwa rasmi na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, katika barua ya Juni 23, 2025.
Barua hiyo ilikuwa na kichwa kinachohusu “Taarifa Rasmi ya Matokeo ya Majadiliano Nje ya Mahakama kuhusu Kumaliza Mgogoro wa Ardhi Na.147/2012 kati ya Huruma Vision, Wananchi na Jiji la Arusha.”
“Tunataka makubaliano hayo yazingatiwe. Haya si maneno ya mtaani, ni makubaliano yaliyoandikwa na Mkurugenzi wa Jiji. Barua yake ya Juni 23, 2025 inaeleza wazi matokeo ya majadiliano yaliyofanyika nje ya mahakama na namna mgogoro ulivyopaswa kumalizika,” amesema Kivuyo.
Amesema wananchi hao walikubali suluhu ya nje ya mahakama baada ya kupewa matumaini kwamba makubaliano yaliyofikiwa yangeheshimiwa na kutekelezwa.
Kwa mujibu wake, awali wananchi hao walikuwa wakidai kupewa ekari tano, lakini katika mchakato wa majadiliano walikubali utaratibu wa kupewa ekari moja pamoja na Sh10 milioni kwa kila mmoja.
“Tumepigania kesi hii kwa miaka 14 kwa fedha zetu. Wengine tumefilisika. Sasa kama Serikali ya Jiji imeandika makubaliano kwamba tutapewa ekari moja na Sh10 milioni kila mmoja kwa gharama tulizotumia, tunataka hayo makubaliano yaheshimiwe,” amesema.
JULAI 15, MSIMAMO WABADILIKA
Hata hivyo, barua ya Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Shaban Manyama, yenye kumbukumbu Na.70.103/01 ‘C’/29, imeongeza utata katika suala hilo.
Barua hiyo inahusu taarifa ya maazimio ya kikao cha Katibu Tawala Mkoa wa Arusha kilichofanyika Julai 15, 2026, kikihudhuriwa na wawakilishi wa Huruma Vision Tanzania, Halmashauri ya Jiji la Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Kwa mujibu wa barua hiyo, kikao kiliazimia kuwa eneo lote la ekari tano libaki chini ya Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa shule.
“Eneo lote (ekari tano) zibaki Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa shule,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Kaimu Mkurugenzi amesema Halmashauri inaendelea na taratibu za kuifuta barua ya Juni 23, 2025 yenye kumbukumbu Na.CAB.70.103/40 na kuwataka wahusika kutotekeleza maelekezo yaliyomo katika barua hiyo hadi watakapoelekezwa vinginevyo.
“TULIONDOLEWA KWENYE MARIDHIANO”
Kwa upande wake, Saruni Olodi, mmoja wa wananchi hao, amesema mgogoro huo ulianza baada ya Huruma Vision Tanzania kupewa takribani ekari 15 za ardhi ya Serikali mwaka 2002, akidai eneo hilo lilitolewa bila kufuata utaratibu.Amesema mwaka 2012 yeye na wenzake saba waliingia katika mgogoro huo baada ya kuwakilisha wananchi katika mkutano wa hadhara kuhusu eneo hilo.
“Tulikuwa tunawakilisha wananchi waliotuletea kama kamati kwenye mkutano wa hadhara. Tulipoenda mahakamani tulijitetea, lakini pia tukamwomba Mkurugenzi wa Jiji ajiunge kwa sababu ardhi ilikuwa ya Serikali,” amesema.
Saruni amesema hukumu ya mwaka 2019 iliipa ushindi upande wao dhidi ya Huruma Vision Tanzania baada ya taasisi hiyo kushindwa kuwasilisha nyaraka halali za kuthibitisha umiliki wa eneo hilo.Amesema baada ya Huruma Vision Tanzania kukata rufaa, shauri hilo liliendelea katika Mahakama Kuu na baadaye Mahakama ya Rufani.
Hata hivyo, anadai wakiwa katika Mahakama ya Rufani walishangazwa kusikia wakili wa Huruma Vision Tanzania akieleza kuwa taasisi hiyo ilikuwa imefikia makubaliano na Halmashauri ya Jiji la Arusha ya kumaliza mgogoro huo.
“Wakili wa Huruma Vision akasema wamekubaliana na Halmashauri ya Jiji. Sisi tukaenda Halmashauri na hata wakili wetu akashangaa kwa sababu hakuwa na taarifa ya makubaliano hayo,” amesema.
EKARI MOJA, SH10 MILIONI KILA MMOJA
Sarun amesema baadaye uliundwa mchakato wa maridhiano, lakini anadai yeye na wenzake waliondolewa kwenye baadhi ya mazungumzo kabla ya kupewa nyaraka zilizokuwa na mapendekezo ya mgawanyo wa eneo.
Kwa mujibu wake, mapendekezo hayo yalihusisha Huruma Vision Tanzania kupata ekari 10 na Serikali kubaki na ekari tano, huku ekari moja kati ya hizo tano ikitengwa kwa ajili ya wananchi hao.
Mbali na ekari hiyo, amesema kila mmoja wa wananchi hao wanane aliahidiwa Sh10 milioni kama sehemu ya gharama walizotumia katika uendeshaji wa kesi hiyo kwa miaka 14.
Hata hivyo, anadai hadi sasa jumla ya Sh40 milioni pekee ndizo zilizolipwa.
“Halmashauri ilituahidi Sh10 milioni kila mmoja kama fidia ya gharama za uendeshaji wa kesi kwa miaka 14. Lakini hadi sasa tumelipwa Sh40 milioni pekee. Wengine hawajalipwa,” amesema.
Sarun amesema ekari hiyo tayari ilipimwa na wananchi hao kupewa nyaraka pamoja na ramani iliyoidhinishwa na mamlaka za ardhi.
“Tumeshapewa ekari moja, limepimwa na tumepata ramani iliyoidhinishwa. Lakini sasa tunaambiwa tusiendeleze eneo hilo. Tunajiuliza, kama tulipewa kihalali, kwa nini leo tunaambiwa tusiliendeleze?” amesema.
WATISHIA KURUDI MAHAKAMANI
Kutokana na mabadiliko hayo, Sarun amesema wananchi hao wanakusudia kurejea mahakamani kuishtaki Halmashauri ya Jiji, wakidai kukiukwa kwa haki walizopata kupitia mchakato wa kesi na makubaliano ya maridhiano.
Amesema wanataka mahakama itoe uamuzi kuhusu uhalali wa hatua zilizochukuliwa na Halmashauri pamoja na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
Pia wameomba Serikali ya Mkoa wa Arusha, Ofisi ya Waziri Mkuu na mamlaka nyingine husika kuingilia kati suala hilo.
“TUNATAKA KUVUNJA CHUNGU”
Katika hatua nyingine, Saruni amesema wananchi hao wanakusudia pia kufikisha suala hilo mbele ya baraza la wazee wa kimila kwa kile alichokiita “kuvunja chungu”, kama sehemu ya utaratibu wa kimila wa kuwasilisha malalamiko kuhusu wanachokiona kuwa ni dhuluma.
Amesema kwa imani ya baadhi ya jamii ya Kimasai, chungu kinachotolewa kwa utaratibu maalumu na baraza la wazee wa kimila kinaweza kuvunjwa kama ishara ya kulaani kitendo kinachoonekana kuwa ni dhuluma.
“Sisi tunataka kufikisha jambo hili kwenye baraza la wazee ili hatua za kimila zitakazofaa zichukuliwe,” amesema.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo anayoitaja ni ya kimila na haipaswi kutafsiriwa kama tishio dhidi ya mtu yeyote.
SH40 MILIONI ZINAIBUA MASWALI
Saruni pia ameibua swali kuhusu Sh40 milioni zilizolipwa katika mchakato huo, akitaka kufahamishwa chanzo cha fedha hizo, utaratibu uliotumika na sababu za baadhi ya wananchi kutolipwa.
“Kuna watu wamepewa Sh10 milioni, jumla Sh40 milioni zimetolewa, lakini wengine hawajapewa. Tunataka kujua hizi fedha zimetoka wapi na kwa nini zimetolewa kwa utaratibu huo,” amesema.
WAFANYABIASHARA 400 HATARINI KUONDOLEWA
Aidha, amesema kuna mpango wa kuwaondoa wafanyabiashara zaidi ya 400 wanaofanya shughuli zao katika soko lililopo eneo hilo.
Amesema wafanyabiashara hao hawajaelezwa watakapohamishiwa iwapo eneo hilo litatumika kwa ujenzi wa shule, akisema hatua hiyo inaweza kuathiri maisha na uchumi wa familia nyingi.
Ameitaka Serikali kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapewa eneo mbadala kabla ya kuchukuliwa hatua yoyote ya kuwaondoa.
“RAIS ATUME TIMU YA UCHUNGUZI”
Kutokana na mvutano huo, Sarun amesema wananchi hao wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda timu maalumu ya uchunguzi kutoka Ikulu ili kuchunguza historia na hatua zote za mgogoro huo.
Wanataka uchunguzi ubaini sababu za Halmashauri kuwaomba kufuta kesi, sababu za wao kuondolewa katika baadhi ya mazungumzo ya maridhiano, msingi wa kutengwa kwa ekari moja, sababu za kutokamilishwa kwa malipo ya Sh10 milioni kwa kila mmoja na kwa nini sasa wanaambiwa wasiendeleze eneo walilopewa.
“Tunaomba kilio chetu kimfikie Mheshimiwa Rais. Aunde timu ya uchunguzi ichunguze kwa nini Halmashauri ilituomba tufute kesi, kwa nini tuliondolewa kwenye mazungumzo wakati kesi ilikuwa yetu, kwa nini tuliahidiwa Sh10 milioni kila mmoja lakini hadi sasa tumelipwa Sh40 milioni pekee, na kwa nini ekari moja tuliyopewa sasa tunaambiwa tusiendeleze,” amesema.
Wananchi hao pia wameomba nafasi ya kukutana na Rais ili kueleza madai yao moja kwa moja na kuomba uchunguzi wa kina.
Kwa sasa, mgogoro huo umeingia katika sura mpya: wananchi wanasisitiza utekelezaji wa makubaliano ya Juni 23, 2025, huku Halmashauri ikisema inaendelea na taratibu za kuifuta barua hiyo na kusisitiza ekari zote tano zibaki kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Halmashauri ya Jiji la Arusha haijatoa ufafanuzi wa kina kuhusu madai ya ekari moja na malipo ya Sh10 milioni kwa kila mmoja, wala sababu za kisheria na kiutendaji za kubadilisha maelekezo yaliyokuwa katika barua ya Juni 23, 2025.
Hatma ya eneo hilo, makubaliano ya nje ya mahakama na madai ya wananchi hao sasa inaweza kuamua iwapo mgogoro huo wa zaidi ya miaka 14 utamalizika kwa maelewano au kurejea tena katika vyombo vya sheria.
Ends






إرسال تعليق