Breaking🔥

KISHINDO ARUSHA KAYOMBO ASHUSHA KIKOSI HATARI CHA WACHEZAJI 127 SHIMISEMITA-MBEYA ,ALENGA KUZOA MAKOMBE YOTE YA MICHEZO 15 , WACHEZAJI WAAGWA KWA MAOMBI MAZITO

ARUSHA YALENGA MAKOMBE YOTE SHIMISEMITA

....Wanamichezo 127 waenda Mbeya, Meya awataka nidhamu, Mkurugenzi: Hakuna kisingizio

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

ARUSHA. Jiji la Arusha limeweka wazi azma ya kutawala michezo ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA), likipeleka wanamichezo 127 kushiriki katika michezo 15 ya mashindano hayo yatakayofanyika Mbeya kuanzia Agosti 16 hadi 29, 2026.

Kikosi hicho kimeagwa kwa kishindo huku viongozi wa Jiji hilo wakitoa kauli nzito ya kutaka kurejea Arusha na makombe yote, wakisisitiza maandalizi yaliyofanyika yamekamilika na hakuna nafasi ya visingizio.

Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, amesema anaamini kikosi hicho kinachoundwa na watumishi wa Jiji kina uwezo wa kufanya vizuri kutokana na maandalizi yaliyofanyika kabla ya safari.

Akiwaaga wanamichezo hao leo Agosti 14,2026 katika jiji la Arusha, Iranghe aliwataka kuzingatia nidhamu, mshikamano na kutumia muda wao kwa ajili ya mashindano, akisisitiza kuwa wanabeba heshima na taswira ya Jiji la Arusha.

“Nidhamu iwe jambo la kwanza. Tunachotaka ni makombe yote ya michezo 15 mnayoenda kushindania myalete Arusha,” alisema.

Meya huyo pia aliwataka wanamichezo hao kuepuka vitendo au mienendo isiyofaa ambayo inaweza kulitia aibu Jiji, akisisitiza kuwa ushindi unapaswa kwenda sambamba na nidhamu.

AFCON 2027 YAINGIA KATIKA MPANGO

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha na Mwenyekiti wa Michezo Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa safari yao si ya kubeba majina yao binafsi pekee, bali pia wanawakilisha Jiji la Arusha.

Rombo alisema utendaji na mwenendo wao Mbeya utakuwa sehemu ya taswira ya Jiji, hasa ikizingatiwa kuwa Arusha inatarajiwa kuwa mwenyeji wa baadhi ya shughuli za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

“Kumbukeni mwakani 2027 kuna mashindano ya AFCON yatakayofanyika hapa Arusha. Ni vyema mashindano haya yakatoa taswira nzuri katika Jiji la Arusha ambako mashindano ya AFCON yatafanyika,” alisema.

Alisema wanamichezo hao wanapaswa kutumia mashindano hayo kuonyesha uwezo, nidhamu na mshikamano ili kulinda heshima ya Jiji.

‘HAKUNA KISINGIZIO’


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alisema Jiji limepeleka timu 15 katika michezo mbalimbali, akidai idadi hiyo inaweza kuwa kubwa ikilinganishwa na majiji mengine nchini.

Kayombo alisema jumla ya wanamichezo 127 watashiriki katika michezo hiyo na kwamba maandalizi yote yamekamilika, ikiwa ni pamoja na mahitaji muhimu ya safari na mashindano.

“Tumejipanga kushinda. Toeni ushindani wa hali ya juu ili mrejee na makombe yote na kuleta sifa katika Jiji la Arusha. Hakutakuwa na kisingizio chochote kwa sababu maandalizi yote yamekamilika,” alisema.

Alisema msafara huo umeondoka Arusha ukiwa na watu 139, wakiwamo wanamichezo na viongozi, ukisafiri kwa mabasi makubwa mawili pamoja na Coaster moja.

Miongoni mwa michezo ambayo Arusha itashiriki ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa kikapu, drafti, bao na michezo mingine, huku jumla ya michezo inayoshirikishwa ikiwa 15.

Kwa kauli za viongozi hao, safari ya Mbeya imebeba zaidi ya ushindani wa michezo; imegeuka kuwa mtihani wa heshima ya Jiji la Arusha, huku kikosi hicho kikiingia uwanjani kikiwa na shinikizo la kutimiza ahadi ya kurejea na “makombe yote.”





Post a Comment

Previous Post Next Post