Breaking🔥

WAKILI MADELEKA ALILIWA KILA KONA ,CHADEMA, ACT-WAZALENDO WAPAZA SAUTI KUKAMATWA KWAKE WATAKA AACHIWE

CHADEMA, ACT-WAZALENDO WAPAZA SAUTI KUKAMATWA KWA MADELEKA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

DAR ES SALAAM. Vyama vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ACT-Wazalendo vimelaani kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka, vikilitaka Jeshi la Polisi kumuachia huru mara moja bila masharti.

Madeleka alikamatwa Agosti 13, 2026, saa 9:30 alasiri katika eneo la Mikocheni B, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kudharau amri ya Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wakili huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo, Agosti 17, 2026, kujibu tuhuma zinazomkabili.

Hatua hiyo imeibua malalamiko kutoka vyama hivyo, ambavyo vimeonya kuwa matumizi ya vyombo vya dola dhidi ya watu wanaotoa maoni kuhusu masuala ya umma yanaweza kuongeza hofu miongoni mwa wananchi na kudhoofisha imani katika taasisi za haki na utawala wa sheria.

Katika taarifa iliyotolewa Agosti 16, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, amesema chama hicho kinataka Madeleka aachiwe mara moja.

“CHADEMA inalitaka Jeshi la Polisi kumuachia huru mara moja bila masharti yoyote. Pia, tunatoa wito kwa wadau wa haki za binadamu, wanasheria, vyombo vya habari na wananchi wote kuendelea kufuatilia kwa karibu suala hili na kuhakikisha haki za Wakili Madeleka zinalindwa,” amesema Rupia.

CHADEMA na ACT-Wazalendo vimesisitiza umuhimu wa vyombo vya dola kuzingatia misingi ya sheria na haki za msingi za mtu anayekabiliwa na tuhuma, huku vikihimiza ufuatiliaji wa karibu wa mwenendo wa kesi hiyo.

Hatua ya kumfikisha Madeleka mahakamani inatarajiwa kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kueleza tuhuma zinazomkabili na kwa upande wa utetezi kujibu kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Post a Comment

Previous Post Next Post