Breaking🔥

SH1.4 BILIONI KUOKOA WATOTO 774,459 DHIDI YA POLIO ARUSHA: NGUVILA AMSHUKURU RAIS SAMIA

Sh1.4 bilioni kuokoa watoto 774,459 dhidi ya Polio Arusha

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

ARUSHA. Serikali imewekeza zaidi ya Sh1.4 bilioni katika uratibu wa kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza kwa watoto (Polio), huku Mkoa wa Arusha ukiweka lengo la kuwafikia watoto 774,459 walio chini ya miaka 10.

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila, amesema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ugonjwa huo na amewataka viongozi na watendaji wote mkoani humo kuhakikisha kila mtoto anayelengwa anapata chanjo.

Dkt. Nguvila alisema hayo jana, Jumatatu Agosti 17, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa kampeni ya chanjo dhidi ya Polio, yanayowakutanisha wataalamu kutoka ngazi ya Mkoa na Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.

Alisema viongozi na watendaji wana wajibu wa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa kampeni hiyo zinatumika kwa ufanisi na thamani ya fedha inaonekana kwa kufikiwa kwa idadi ya watoto iliyolengwa.

“Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna kubwa anavyowapenda Watanzania, kuwajali na kulinda afya za watu wake anaowaongoza. Hii ni dhahiri kuwa Dkt. Samia anapenda, angependa na ataendelea kupenda afya zetu ziwe salama,” alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Nguvila, kampeni hiyo itatekelezwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, kliniki mkoba, shule za msingi pamoja na ngazi ya kaya, ili kuhakikisha watoto wanaolengwa hawakosi huduma hiyo.

Chanjo ni kinga na uwekezaji wa Taifa

Dkt. Nguvila alisema chanjo dhidi ya Polio si suala la afya pekee, bali ni sehemu ya usalama na uwekezaji katika kizazi kijacho, akieleza kuwa watoto wenye afya bora ni msingi wa ujenzi wa Taifa lenye nguvu.

Alisema kuzuia Polio kunasaidia kuwaepusha watoto na madhara ya kupooza, huku pia kukipunguzia Serikali gharama kubwa ambazo zingetumika katika matibabu na huduma kwa watu wenye ulemavu.

“Afya za watoto zikiimarika, tutakuwa tumeweka msingi wa kujenga Taifa bora la kesho. Ni muhimu kuhakikisha tunawakinga watoto wetu dhidi ya ugonjwa huu,” alisema.

Viongozi wa jamii watakiwa kuongoza kampeni

Aidha, aliwataka viongozi wa Serikali na jamii kuanzia vitongoji, mitaa, vijiji, kata na wilaya kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo.

Aliwataka pia viongozi wa kimila, viongozi wa dini pamoja na viongozi wengine wa kuchaguliwa na kuteuliwa kushirikiana na wataalamu wa afya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo.

Dkt. Nguvila alisema ushirikishwaji huo ni muhimu katika kuondoa dhana potofu na imani zinazoweza kuwafanya baadhi ya wazazi au walezi kusita kuwapeleka watoto kupata chanjo.

Mafunzo hayo yanawahusisha wataalamu wa afya kutoka Halmashauri, Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Maafisa Elimu wa Halmashauri, na yanaendeshwa kwa siku mbili kwa kuwezeshwa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya.





Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post