Breaking🔥

PIC YAITAKA TANAPA KUONGEZA UWEKEZAJI, MAZAO MAPYA YA UTALII

PIC YAITAKA TANAPA KUONGEZA UWEKEZAJI, MAZAO MAPYA YA UTALII

Na Joseph Ngilisho | DODOMA


DODOMA. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Serikali, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kuimarisha uwekezaji katika hifadhi za taifa kwa kuboresha miundombinu na kuanzisha mazao mapya ya utalii.

Kamati hiyo imesema hatua hizo ni muhimu katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kukuza mapato yatokanayo na sekta hiyo, ambayo ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato ya Taifa.

Maelekezo hayo yalitolewa Agosti 13, 2026 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Rashid A. Shangazi, wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Dodoma kujadili utekelezaji wa miradi ya uwekezaji katika hifadhi za taifa, masuala ya uhifadhi na mikakati ya kukuza utalii nchini.

Shangazi alisisitiza umuhimu wa TANAPA kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati inayolenga kuongeza thamani ya maeneo ya hifadhi, ikiwamo kuboresha miundombinu ya utalii na kuibua fursa na bidhaa mpya zitakazowavutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo, uwekezaji katika miundombinu na ubunifu wa mazao mapya ya utalii unapaswa kwenda sambamba na jitihada za kuhifadhi rasilimali za Taifa ili sekta hiyo iwe endelevu na iendelee kutoa mchango mkubwa katika uchumi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nkoba E. Mabula, pamoja na viongozi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina na Menejimenti ya TANAPA iliyoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Massana G. Mwishawa.

Kamati ya PIC ni miongoni mwa Kamati za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye jukumu la kusimamia na kutoa ushauri kuhusu mwenendo wa uwekezaji wa mitaji ya umma katika mashirika, kampuni na taasisi za umma zilizo chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta tija, unazalisha mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku ukizingatia maslahi mapana ya Taifa.

 




Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post