TANROADS YAMHAKIKISHIA RC MAKALA KASI UJENZI WA UWANJA WA NDEGE LAKE MANYARA WAFIKIA ASILIMIA 9,MKAMDARASI ALIPWA HADAI KITU

TANROADS: Ujenzi wa Upanuzi wa Uwanja wa Ndege Lake Manyara Wafikia Asilimia 9

Na Joseph Ngilisho |KARATU

MENEJA wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnaid Masawe, amesema utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Lake Manyara wilayani Karatu umefikia asilimia tisa, huku mkandarasi akiwa tayari amelipwa zaidi ya Sh bilioni 14.

Mhandisi Masawe amesema hayo Agosti 27, 2026, wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ya kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema hadi sasa mkandarasi amelipwa malipo ya awali ya Sh bilioni 12.89 pamoja na Sh bilioni 1.85 kupitia Cheti cha Kwanza cha Malipo, hatua inayofanya malipo yaliyofanyika kufikia takribani Sh bilioni 14.74.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masawe, mpango kazi wa mradi ulilenga kufikisha utekelezaji katika asilimia 14 kwa hatua hiyo, hivyo kiwango cha sasa cha asilimia tisa bado kiko chini ya matarajio yaliyowekwa.

“Mpaka sasa mkandarasi amelipwa malipo ya awali ambayo ni Sh bilioni 12.89, lakini pia amelipwa Cheti cha Kwanza cha Malipo cha Sh bilioni 1.85,” amesema.

Hata hivyo, Mhandisi Masawe amesema mkandarasi tayari ametekeleza takribani asilimia 73 ya kazi zilizopo katika hatua ya mkataba, huku vifaa vingine vikitarajiwa kuwasili baada ya kukamilika kwa kazi za awali za ujenzi.

Amesema kazi zinazoendelea ni sehemu muhimu ya maandalizi ya upanuzi wa uwanja huo, unaolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia usafiri wa anga na kuchochea zaidi shughuli za utalii katika maeneo yanayozunguka Ziwa Manyara na wilaya ya Karatu.



 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafiri kwa watalii wanaokwenda katika hifadhi na maeneo ya utalii, sambamba na kuongeza wigo wa aina na ukubwa wa ndege zitakazoweza kutua katika uwanja huo.

Amesema uwanja huo utakapokamilika utaweza kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 40, huku uwekaji wa taa na lami ukitarajiwa kuongeza usalama na kuwezesha ndege kutua kwa uhakika wakati wa usiku.

“Faida za mradi huu ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii na abiria. Pia utaongeza aina na idadi ya ndege, ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 40. Zaidi, uwepo wa taa utaongeza usalama na uhakika wa ndege kutua, kwani taa na lami vitasaidia kuongeza usalama,” amesema CPA Makalla.

CPA Makalla amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa Sh bilioni 88 unaolenga kuboresha uwanja huo, akisema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa sekta ya utalii na usafiri wa anga mkoani Arusha.

Aidha, amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliowekwa katika mkataba, ambao unatarajiwa kufikia Juni 2027.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha uwanja huo unakuwa tayari kutumika kabla ya mashindano ya AFCON 2027, yatakayofanyika Tanzania kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imelenga pia kubaini changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi na kuzingatia viwango, muda na masharti ya mkataba.

Post a Comment

Previous Post Next Post