TANROADS YAKANUSHA MADAI YA FIDIA, YASEMA MWENYE NYUMBA YUPO NDANI YA HIFADHI YA BARABARA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha umekanusha madai ya mkazi wa eneo la Tandoro, Yusufu Hamed, aliyedai kuwa ametakiwa kubomoa nyumba yake kupisha ujenzi wa barabara bila kulipwa fidia, ukieleza kuwa nyumba hiyo ipo ndani ya hifadhi ya barabara na hivyo haistahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Madai ya Yusufu yalitokana na malalamiko yake kuwa alifanyiwa tathmini ya mali zake na kuwasilisha nyaraka mbalimbali za umiliki wa eneo hilo, lakini hadi sasa hajalipwa fidia licha ya kutakiwa kuondoa nyumba yake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhandisi anayesimamia mradi huo, Sande Boaz, alisema vipimo rasmi vya eneo hilo vinaonesha nyumba ya Yusufu ipo ndani ya hifadhi ya barabara, jambo linalomfanya asiwe miongoni mwa wananchi wanaostahili kulipwa fidia.
Alisema wananchi waliokuwa ndani ya eneo lililostahili fidia walifanyiwa tathmini, wakalipwa stahiki zao na kuondoka kupisha mradi, huku waliobaki ndani ya hifadhi ya barabara wakitakiwa kuondoa majengo yao kwa hiari kufuatia notisi walizopewa.
"Tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi kupitia viongozi wa maeneo yao na mikutano mbalimbali. Wengi wameelewa na tayari wamebomoa nyumba zao au wamehamia nyuma ya mipaka ya hifadhi ya barabara," alisema Boaz.
Aliongeza kuwa TANROADS imeendelea kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuondoa majengo yao kwa hiari kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Boaz alisema uwepo wa nyumba ndani ya hifadhi ya barabara unaendelea kuchelewesha uhamishaji wa miundombinu muhimu ikiwemo mabomba ya maji na nguzo za umeme, hali inayokwamisha maendeleo ya mradi huo.
Alisisitiza kuwa wananchi wote waliolipwa fidia walikuwa nje ya hifadhi ya barabara kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa, huku akieleza kuwa hakuna mtu anayenyimwa fidia endapo anatimiza vigezo vinavyotakiwa kisheria.
Aidha, aliwataka wananchi ambao bado hawajaondoa majengo yao kushirikiana na Serikali ili kuruhusu utekelezaji wa mradi huo, akisema barabara hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Arusha na watumiaji wengine wa barabara.
"Tunaomba wananchi waunge mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuondoka kwenye hifadhi ya barabara ili ujenzi ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika na miundombinu bora," alisema Boaz.
ENDS..

Post a Comment