Breaking🔥

POLISI YAMKAMATA NEEMA MUSHI,MFANYABIASHARA ARUSHA ALIYEMCHOMA NA PASI YA UMEME KIJAKAZI NA PASI

 POLISI YAMKAMATA MFANYABIASHARA ARUSHA KWA TUHUMA ZA KUMCHOMA KIJAKAZI NA PASI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mfanyabiashara, Neema Ngalami Mushi, kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mfanyakazi wake wa ndani mwenye umri wa miaka 16 kwa kumchoma na pasi ya umeme, baada ya kuzuka sintofahamu kuhusu fedha za mauzo ya kipande cha keki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa na kusema anaendelea kuhojiwa huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.

"Polisi walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa. Kwa sasa anaendelea na mahojiano na mara upelelezi utakapokamilika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa," amesema Kamanda Masejo.

Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa ni mmiliki wa duka la nguo lililopo eneo la Makao Mapya, jijini Arusha, ambako binti huyo alikuwa akifanya kazi.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari, mwathirika huyo alidai tukio hilo lilitokea Jumamosi baada ya mteja kununua kipande cha keki kilichokuwa kikiuzwa dukani kwa Sh500 na kumkabidhi noti ya Sh5,000 huku akiwa hana chenji ya kumrudishia.

Amedai baada ya kumweleza mwajiri wake kuhusu hali hiyo, badala ya kutafutiwa suluhisho, alituhumiwa kuficha fedha hizo na baadaye kushambuliwa kwa kuchomwa na pasi ya umeme sehemu mbalimbali za mwili, hali iliyomsababishia majeraha.

Tukio hilo limeibua hisia kali kwa wananchi na watetezi wa haki za watoto, huku Jeshi la Polisi likisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post