OLE MILLY: SERIKALI IBEBE BENDERA YA TANZANITE, WANANCHI WAPATE MANUFAA
Na Joseph Ngilisho |, SIMANJIRO
Ole Millya alitoa kauli hiyo wakati akizungumza baada ya ziara ya Waziri wa Madini katika eneo la Mererani, Simanjiro, ambapo alisema ujio wa viongozi wa Serikali katika eneo hilo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kusikiliza changamoto za wachimbaji, wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea sekta hiyo.
Alisema Tanzanite ina upekee mkubwa duniani kwa kuwa inapatikana katika eneo la Mererani pekee, hivyo Serikali inapaswa kuweka mkakati maalumu wa kuhakikisha madini hayo yanatumika ipasavyo kuongeza thamani ya uchumi wa Taifa.
“Kwa sababu tunajua jina la Tanzania, Mheshimiwa Waziri, ni vyema tukaangazia macho yetu na kubeba bendera ya nchi kwa madini haya,” alisema Ole Millya.
Alisema Serikali inapaswa kuangalia kwa upana mnyororo mzima wa thamani wa Tanzanite, kuanzia uchimbaji, upatikanaji wa mitaji, ununuzi, uongezaji thamani hadi masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, uchimbaji wa Tanzanite una gharama kubwa na baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakitumia muda mrefu kuwekeza katika migodi hiyo, hivyo hatua za kuboresha sekta hiyo hazipaswi kuathiri mitaji na uwekezaji wa wachimbaji.
Ole Millya alisema Serikali inapaswa kusikiliza maoni ya wachimbaji wadogo, wafanyabiashara, wanawake wanaojishughulisha na biashara ya madini na wadau wengine ili kuweka mfumo utakaonufaisha Taifa bila kuwaumiza wanaowekeza katika sekta hiyo.
Akimpongeza Waziri wa Madini kwa ziara hiyo, alisema kitendo cha kuendelea kukutana na wananchi na kusikiliza changamoto zao ni ishara ya Serikali inayoweka maslahi ya wananchi mbele.
Alisema hata muda ambao Waziri ametumia Mererani, licha ya kuwa katika ziara tangu asubuhi, unaonyesha dhamira ya Serikali ya kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
“Tumekabidhiwa dhamana ya kuwahudumia wananchi. Hii ndiyo maana ya Serikali; kusikiliza wananchi, kuelewa changamoto zao na kuhakikisha mwisho wa siku wanapata furaha na manufaa ya rasilimali zilizopo nchini,” alisema.
Ole Millya pia alisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaifahamu vizuri historia ya Tanzanite na juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta hiyo, akisema hatua zaidi zinahitajika sasa kuhakikisha madini hayo yanakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa.
Alisema wananchi wa Simanjiro wako tayari kushirikiana na Serikali katika kutekeleza maelekezo yatakayotolewa kwa lengo la kuboresha uchimbaji na biashara ya Tanzanite.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kulinda na kukuza sekta ya madini, hususan Tanzanite, ambayo imekuwa sehemu muhimu ya utambulisho wa Tanzania kimataifa.
Aidha, viongozi hao waliwahimiza watendaji wa Serikali katika sekta ya madini kuendelea kufanya kazi kwa weledi, huku wakitambua changamoto zinazowakabili katika kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Ole Millya aliwahakikishia wananchi wa Simanjiro kuwa viongozi wao wataendelea kuwa sehemu ya jitihada za Serikali katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili na kuhakikisha Tanzanite inakuwa rasilimali yenye manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ends..


Post a Comment