Breaking🔥

MTOTO WA MIAKA 5 AUAWA BAADA YA KUTEKWA, WATEKA NYARA WADAI MILIONI 7

MTOTO WA MIAKA 5 AUAWA BAADA YA KUTEKWA, WATEKA NYARA WADAI MILIONI 7

Na Joseph Ngilisho | SIMIYU

MTOTO wa kiume mwenye umri wa miaka mitano, Samike Mponeja, mkazi wa Kijiji cha Gulumwashi, Kata ya Malampaka, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, amekutwa amefariki dunia baada ya kutekwa nyara na watu wanaodaiwa kudai Sh milioni saba kutoka kwa familia yake.

Samike aliripotiwa kutoweka Agosti 6, 2026, akiwa machungoni pamoja na watoto wenzake. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo waliwalaghai watoto hao kwa kuwatuma nyumbani, na waliporejea eneo la malisho hawakumkuta Samike.

Jitihada za kumtafuta mtoto huyo ziliendelea kwa siku kadhaa, hadi Agosti 19, 2026, mwili wake ulipogunduliwa ukiwa juu ya mti katika eneo hilo.

Tukio hilo limezua huzuni na mshtuko mkubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Gulumwashi na maeneo ya jirani, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira halisi ya tukio hilo na waliohusika.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, amesema watu watatu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo tayari wamekamatwa na Jeshi la Polisi.

Amesema watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa wakati uchunguzi ukiendelea, huku taratibu za kisheria zikifuatwa ili kuhakikisha waliohusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Tukio hilo limeongeza hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, hasa wazazi na walezi, kuhusu usalama wa watoto wanapokuwa nje ya makazi yao.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم