KAMPUNI YA ALGERIA KUJENGA VIWANDA VITATU VYA KOROSHO TANZANIA
By Arushadigital
KAMPUNI ya ubanguaji na usindikaji wa korosho ya Sarl Anacard’Or kutoka Algeria, imepanga kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vitatu vya kisasa nchini Tanzania, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo na kukuza ushindani wake katika soko la dunia.
Mpango huo umetangazwa na Mmiliki na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Walid Dib, alipokutana na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, wakati wa ziara ya balozi huyo katika kiwanda cha kampuni hiyo jijini Oran.
Dib alisema kampuni hiyo imevutiwa na ubora wa korosho inayozalishwa Tanzania na imeamua kupanua shughuli zake kwa kuanzisha viwanda nchini, huku kiwanda cha kwanza kikitarajiwa kujengwa Masasi mkoani Mtwara.
“Korosho ya Tanzania ina ubora wa kipekee na tumeamua tujenge viwanda vitatu, tukianzia na cha Masasi mkoani Mtwara, kitakachotumia mashine za kisasa kutoka Vietnam,” alisema Dib.
Alisema tayari kampuni hiyo, kwa kushirikiana na mbia wa ndani, ipo katika hatua za kukamilisha usajili wa kampuni ya kwanza itakayofanya shughuli hizo nchini kwa jina la Kilimanjaro Nuts Limited.
Dib alisema pia kampuni hiyo imeanza maandalizi ya kuanzisha maghala ya kuhifadhia korosho wilayani Masasi na inatarajia kuagiza mashine kutoka Vietnam mwezi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dib, mashine hizo zinatarajiwa kuwasili nchini pamoja na wataalamu kutoka Vietnam, ambao wataanza kutoa mafunzo kwa wataalamu na wafanyakazi wa Tanzania kuanzia Januari 2027.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi Matinyi alimpongeza Dib kwa uamuzi wa kuwekeza nchini na kumhakikishia kuwa Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha mpango huo.
Alisema uwekezaji huo utasaidia kuongeza ajira, mapato ya Serikali, ujuzi wa ndani na upatikanaji wa fedha za kigeni, huku ukiongeza thamani ya korosho kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.
“Ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa uwekezaji wa viwanda vya ubanguaji unaongezeka nchini ili kulipa thamani zaidi zao hili kabla ya kuuzwa nje na kupunguza uuzaji wa korosho ambazo hazijabanguliwa,” alisema Matinyi.
Dib pia alieleza mafanikio ya kampuni yake katika biashara ya korosho ya Tanzania, akisema sasa ameamua kuelekeza ununuzi wake kwa korosho kutoka Tanzania kutokana na ubora wake.
Alimwonesha Balozi Matinyi korosho za Tanzania zilizopitia hatua 11 za uzalishaji katika kiwanda hicho hadi kufungashwa na kuwa tayari kwa kuuzwa katika soko la kimataifa.
“Nilipokea makontena sita mwezi uliopita; sasa hivi nina mengine sita bandarini Oran, huku saba yakiwa njiani baharini na mengine saba bandarini Dar es Salaam yakisubiri kuanza safari. Kila kontena limebeba tani 27 za korosho,” alisema.
Akihitimisha ziara yake katika kiwanda hicho, Balozi Matinyi alisema juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) zimeendelea kuchochea ukuaji wa uzalishaji na kuongeza thamani ya zao hilo.
Alisema Tanzania ilizalisha tani 617,683 za korosho katika msimu wa 2025/26, ambazo ziliingiza Sh1.25 trilioni, na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa korosho duniani baada ya Côte d’Ivoire, Vietnam na India.
Uwekezaji huo wa kampuni ya Sarl Anacard’Or unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kusindika korosho ndani ya nchi, kuongeza ajira na mapato, pamoja na kupunguza utegemezi wa kuuza zao hilo ghafi katika masoko ya kimataifa.



إرسال تعليق